Ukweli wa Mambo: Sera ya Kitaifa Ardhi-Gangaganga za Mganga

SERA YA KITAIFA YA ARDHI – GANGAGANGA ZA MGANGA
Makala ya Nguvu ya Hoja kwa KSB Jumamosi 5.12.2009
na Ndugu Mwandawiro Mghanga

Gangaganga za mganga humpa mgonjwa matumaini ya kupona. Bali kuna tofauti ya matumaini ya kupona ambayo yanaweza kumuongezea mgonjwa muda wa kuishi na kupona kwenyewe hasa. Mara nyingi tume mbalimbali ambazo huundwa na Serikali mara kwa mara kuhusu maswala tilatila, mkiwemo ya ardhi, zimekuwa gangaganga za mganga tu ambazo zimewapa wananchi matumaini ya bure kwamba swala nyeti la ardhi linashughulikiwa na kuletewa ufumbuzi wa kudumu.

Kumbe mapendekezo yanayofanywa na tume za ardhi kama ile ya Njonjo na ya Ndung’u hayatekelezwi hata chembe wala hayakusudiwi kutekelezwa. Na hii ni baada ya kutumia mamilioni ya fedha za umma. Badala yake kunaendelea kuundwa tume juu ya tume zote zikiwa na nia za kupoesha harakati za umma za kudai ukweli na haki. Katika historia ya Kenya tume zimekuwa mbinu za Serikali za kuwasukia na kuwavalisha vilemba vya ukoka hususani makabwela wanaodai haki juu ya ardhi na maliasili.

Majuma machache yaliyopita tumepokea habari nzuri kwamba kuwa sera ya kitaifa ya ardhi hatimaye imepitishwa na Baraza la Mawaziri. Kwa sababu swala la ardhi ni nyeti, imechukua muda mrefu mno kutoka sera hiyo iandikwe hadi ipitishwe na Baraza la Mawaziri. Na bado, hakuna sera ya kitaifa ya ardhi nchini. Maana lazima ijadiliwe na kupitishwa na Bunge. Kutokana na mapendekezo yaliyoko ndani ya sera hii ya kitaifa ya ardhi, mengine yakikaribia kuwa ya kimapinduzi, sioni jinsi itakavyopewa kipaumbele na bunge hili lilojaa makabaila. Na hata ikijadiliwa, sioni jinsi itakavyopitishwa. Na ikipitishwa itakuwa imevunjwa makali na kubaki kifuu kitupu ambacho hakifai sumni kwa masilahi ya Wakenya wengi wanaolilia ardhi. Na hata sera hii ikipitishwa pasina mabadiliko, sioni sera ya ardhi ya kitaifa ikitekelezwa na Serikali hii kwa masilahi ya kitaifa na ya makabwela wengi ambao wanahitaji ardhi ya kuzalisha chakula, makao na mahitaji mengine muhimu. Wala sioni jinsi Serikali iliyoko ambayo inaongozwa na makabaila wanaomiliki maelfu ya maekari ya ardhi kila pahali nchini itakubali kutekelezwa kwa Sera ya kuwanyang’anya ukiritimba wa ardhi ambao umewafanya na unaendelea kuwafanya mamilionea na mabilionea. Si rahisi kumnyang’anya mbwa mfupa wa nyama uliyoko mdomoni. Tena tunajua kinyozi hajinyoi na akijinyoa hujikata.

Dalili ya mvua ni mawingu na mwanzo wa ngoma ni lele, kama Waziri wa Ardhi ana nia na uwezo wa kutekeleza sera ya ardhi basi angelikuwa anaendelea kutekeleza mapendekezo ya tume ya ardhi ya Ndung’u yanayohusu ardhi ya umma iliyonyakuliwa na watu binafsi kote nchini. Lakini kwa sababu mapendekezo ya tume ya Ndung’u yamewahusisha vigogo, baadhi yao wakiwa viongozi wa Serikali, katika unyakuzi wa ardhi ya umma, haijatekelezwa hadi sasa. Isitoshe, mbona kinyang’anyiro cha ardhi kinaendelea Pwani na kote nchini kuliko wakati wowote mwingine? Ukweli wa mambo ni kwamba sera yoyote ya kuleta haki na usawa nchini haiwezi ikatekelezwa na Serikali inayoongozwa na wanaofaidi kutokana na dhuluma na ufisadi. Tangu lini fisi akajihukumu kwa kosa la kumla mwanambuzi?

Sera ya kitaifa ya ardhi ni muhimu na inahitajika sana maana itatoa mwelekeo kuhusu mfumo wa umilikaji wa ardhi na jinsi ardhi itapangwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo. Hivi sasa kuna sheria nyingi mno za ardhi ambazo zinakinzana na kutatanisha. Kupitia kwa sera ya kitaifa ya ardhi ama katiba mpya ya kitaifa kunaweza kuundwa sheria chache tu ambazo zitatoa mwelekeo wazi na bayana uliyo madhubuti wa kutatua maswala ya ardhi mahakamani.

Sera yoyote ya ardhi ya kimaendeleo sharti izingatie kwamba ardhi ni mali ya kitaifa, ya vizazi vya sasa na vijavyo na hivyo basi kila raia ana haki na jukumu ya kuitumia, kuifaidi na kuihifadhi. Si sahihi kuendelea kuwa na wananchi wasiyo na haki ya hata inchi ya nchi yao. Ardhi inafaa kupangwa, kutumiwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya kuzalisha mahitaji ya chakula, nguo, makazi na mambo yote muhimu na ya kimsingi ya kila raia wala si kwa ajili ya ulanguzi na walanguzi. Si sahihi kuendelea kuwa na jamaa zenye kumiliki mamia ya maelfu ya ekari ya ardhi wakati wengi wanakosa hata ardhi ya kujengea jamaa zao na kuwalimia chakula. Swala la maskwata linahitaji kuondolewa huku mikakati mahusisi ya kuondoa mitaa ya mabanda ikihitajika kufanywa na kutekelezwa. Wakati umefika wa kutekelezwa kwa mipango ya matumizi ya ardhi yenye lengo la kufanya miji yetu kuwa misafi, ya kupendeza na ya ustaarabu. Aidha, jamii za nchi yetu zipewe uwezo wa kusimamia ardhi na rasilimali za ardhi kwenye maeneo yao huku ardhi ikipewa wale wanaoifanyia kazi kwa mahitaji muhimu ya jamaa na taifa.

Bali haya yote ni mapendekezo. Na nchi hii haina upungufu wa mapendekezo na sera. Kenya ina ukame wa maongozi na viongozi wenye nia na ujasiri wa kutekeleza sera za kuhakikisha kuwa kila Mkenya anafaidi kutokana na ardhi na maliasili ya Kenya. Viongozi wa sasa, wanaoongozwa na tamaa na shauku za utajiri wa kibinafsi, wana haja na kutumia ardhi na mali asili kujitajirisha wao na jamaa na marafiki zao tu. Hawajali makabwela wala masilahi ya kitaifa. Ili kuleta na kutekeleza sera ya kitaifa ya ardhi ya kimaendeleo, hatuna budi kuwaondoa na badala yake kuwaweka uongozini wazalendo wenye kuongozwa na itikadi ya ujamaa yenye msingi katika masilahi ya umma.

Mwandawiro Mghanga, Barua pepe: mwandawiro2002@yahoo.com

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.