Ukweli wa Mambo:Pesa ya Uma Si Mali ya Binafsi
Ukweli wa Mambo is a KSB series that began in 2007 and that features postings and articles created by or through Ndugu Mwandawiro Mghanga, former MP of Wundanyi constituency. Mwandawiro was exiled in Sweden before he returned to Kenya to participate in local politics. We continue with this series in Kiswahili, Kenya’s National language.
NA HAKI ITENDEKE MARA MOJA
Makala ya Nguvu ya Hoja kwa KSB Jumamosi
na Ndugu Mwandawiro Mghanga
Habari kwamba Serikali imetenga shilingi milioni thelathini na tatu kwa ajili ya kukarabati nyumba za binafsi za Waziri Mkuu ni za kushangaza, kushtusha, kutisha, kuhofisha na kukasirisha. Labda ni tetesi zisizo na ukweli zinazosambazwa na vyombo vya habari. Pamoja na ufisadi uliyokolea nchini na ulafi wa pesa na mali wa viongozi wa nchi hii, sikutarajia kwamba hili lingelifikirika, kusadikika au kufanyika, tena hadharani na bila haya wala aibu. Bali penye moshi hapakosi moto na lisemwalo lipo na likiwa halipo li njiani linakuja.
Tulikuwa tunalaani ufisadi uliyonoga na kunawiri nyakati za utawala wa Moi, kumbe ukishangaa ya Musa utaona ya firauni! Pesa za Serikali ni pesa za umma na kamwe hatuwezi kukubali zigeuzwe mali ya binafsi na kutumiwa vururumtende. Kutumia pesa za umma kwa masilahi ya kibinafsi ni udanganyifu, wizi, ufisadi na uhalifu. Haiwezi kuwa vingine. Kuchukua milioni thelathini na tatu ya pesa za umma na kuzitumia kukarabati nyumba za binafsi za Waziri Mkuu bila shaka ni kupora mali ya umma. Tena, haijalishi ni kiasi gani, mali ya umma ni mali ya umma hata ikiwa ndururu, hivyo si haki au halali ibinafsishwe. Waziri Mkuu akikubali kukarabatiwa nyumba zake za binafsi na pesa za umma basi atakuwa amekubali kushiriki uhalifu. Ushauri wangu ni akarabati mali yake na pesa zake, najua anaweza. Asikubali kushiriki katika kujenga utamaduni huu wa kuhalalisha wizi, ufisadi na uporaji wa ushuru wa raia.
Ikiwa Bunge limekubali kuidhinisha pesa za umma kutumiwa kukarabati nyumba za binafsi za Waziri Mkuu, ama mtu yoyote, basi limewasaliti wananchi wa Kenya na vilevile limeshiriki katika jinai. Nikisema hivi, naamini kuwa Waziri Mkuu ana haki ya kuwa na maskani ya kustahili wadhifa wake na majukumu yake ya kitaifa. Maskani yake yanaweza kugharimu hata milioni mia moja au zaidi. Ajengewe majumba hayo, lakini bora tu yawe mali ya Serikali ambayo atayatumia hadi atakapomaliza kazi yake. Lakini kutumia mali ya umma kumjengea ama kumakarabatia mtu yoyote yule nyumba zake binafsi zitakazorithiwa na jamaa yake si sahihi hata kidogo.
Rais mstaafu, Daniel Arap Moi, hangelipewa majumba ya Serikali yaliyoko Kibera aliyokuwa akiyatumia akiwa rais. Hiyo ilikuwa mali ya umma na ni makosa yazawadiwe mtu binafsi hata awe nani. Angehamia majumba yake binafsi na kuyaacha majumba hayo kutumiwa kwa shughuli za Serikali. Je, tukijenga utamaduni wa viongozi kurithi mali ya umma, si Rais anaweze kutarajia kurithi hata ikulu ya Rais atakapomaliza muda wake? Aidha, tamaa ya kujilimbikizia mali ikiwa ni pamoja na ya wizi, itawapeleka wapi?
Tukiacha haya ya tamaa mbele mauti nyuma, tugusie ya haki na sheria. Nayo sheria ni msumeno, hukata mbele na nyuma. Habari kuu za kila siku ni kuhusu ikiwa watu, mkiwemo viongozi wa nchi, ambao wanatuhumiwa kwa kupanga, kuchochea na kudhamini ghasia za baada ya uchaguzi, watashtakiwa hapa nchini, huko Uholanzi ama wataundiwa tume ya ukweli, haki na maridhiano. Baraza la Mawaziri linababaika wala halina mwelekeo. Nani atakuwa pweza wa kujikanga na mafuta yake mwenyewe? Shinikizo kubwa zaidi za haki na kisheria zinazotingisha nakutetemesha Serikali hii ni zile za kutoka nje, za kibeberu. Walisaini Mkataba wa Roma, nao Mkataba wa Roma na Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa ni ukolonimamboleo. Kenya si huru tena, inaongozwa na mikataba na sheria za kibeberu.
Viongozi wanaouabudu ubeberu hadi kusaliti nchi kwa kukubali majasusi na polisi wa kigeni kuingia huku kuwakamata, kuwahoji, kuwatesa, kuwateka hadi nchi za kigeni na hata kuua wananchi, sasa wenyewe wanaandamwa na mabeberu. Kumbe mchimba kisima huingia mwenyewe. Siwahurumii maana hawana huruma hata kidogo hawa vigogo watuhumiwa. Bali naona uchungu kwa nchi yetu ambayo imefikishwa kwa hali ya kupoteza uhuru wa kitaifa. Serikali gani inayokubali kusomewa na kukemewa na mabalozi wa kigeni usiku na mchana?
Ndiyo, wazimu huu lazima uwe na kikomo. Uhalifu ni uhalifu, bahasha ifunguliwe na watuhumiwa wajulikane, wakamatwe, wawekwe korokoroni na kushtakiwa nchini, huko Uholanzi ama popote pale. Watuhumiwa wenye vyeo serikalini waondoke ama waondolewe na kufuata wenzao korokoroni na mahakamani. Hii ndiyo sheria na haki yao wenyewe, wanaitumia kwa makabwela bali leo imewafikia. Mwosha huoshwa. Tusikubali tume ya ukweli, haki na maridhiano yenye shabaha ya kuwasamehe na kuwawachilia waliyopanga na kutekeleza njama za kuwaua wengine maksuudi. Ikiwa tutawasamehe wahalifu wa ghasia za baada ya uchaguzi basi basi tuwasamehe wahalifu wote, tuwafungue wafungwa wote nchini na kuanza upya. Njama za mwamba ngozi kamba kuvutia kwake hatuzitaki.
Jambo la muhimu zaidi ni kwamba chochote kile kinachohitajika kufanywa ili kuiondoa Serikali hii kutoka madarakani kwa njia za kidemokrasi, kifanyike haraka iwezekanvyo. Serikali hii imechafuka kadamnasi ya wananchi na kimataifa Isitoshe imeshindwa kulinda uhuru wa kitaifa. Na inende kunenda!
Mwandawiro Mghanga, Barua pepe: mwandawiro2002(at)yahoo.com