Ukweli wa Mambo: Maisha Chini ya Ubepari Imechosha Uma
UMMA UMECHOSHWA NA MAISHA CHINI YA MFUMO WA UBEPARI
Makala ya Nguvu ya Hoja kwa KSB Jumamosi 18.12.2009
na Ndugu Mwandawiro Mghanga
Penye moshi bila shaka hapakosi moto. Miaka aroboani na sita tangu tujinyakulie uhuru kutoka kwa ukolonimkongwe wa Wingereza dalili zinaonyesha kuwa umma umechoka na maisha chini ya mfumo wa ubepari. Na kama kuna pahali ukweli huu unajihidhirishia basi na katika Siku Kuu za Kitaifa, Madaraka Dei, Kenyatta Dei ambayo kwa kweli inafaa kuitwa Siku ya Mashujaa wa Kitaifa, na Jamhuri Dei. Pia na sherehe zingine za kitaifa kama Leba Dei.
Katika makumi ya sitini baada tu ya uhuru mnamo mwaka wa 1963, wananchi walikuwa wakimiminika kusherehekea Siku Kuu za Kitaifa kwa fahari, vifijo na nderemonderemo. Nyimbo ziliimbwa, ngoma zilicharazwa na kuchezwa, michezo mbalimbali iliburudisha, hotuba zilitolewa na viongozi kwa ufasaha na zikapokelewa na umma kwa mishangilio ya furaha na bashasha. Baadae karamu ziliandaliwa kila pahali. Almradi, Wakenya walikumbuka historia yao ya mapambano dhidi ya ubeberu huku wakiwa na matumaini makubwa kwamba maisha yao yangeliboreka, kama si wakati huo basi ni katika siku za usoni. Na kwa kweli katika kipindi cha miaka michache baada ya uhuru wananchi walishuhudia mipango mizuri yenye kuwahamasisha na kuwapa matumaini. Sera kabambe za kuimarisha uchumi wa kilimo, biashara na viwanda na za kuleta ajira kwa wengi zilitekelezwa. Huduma za jamii kama elimu, matibabu, nyumba na burudani zilionekana zikikua sehemu nyingi nchini, mijini na mashmbani.
Lakini kumbe mgema akisifiwa pombe hulitia maji, sera za kimaendeleo hazikudumu muda mrefu. Siasa za hiana na ulafi zilitibua mambo na kufanya matumaini ya umma kuanza kuyeyuka kama matofali ya barafu. Mana viongozi walipoteza rada huku wakisahau lengo la kupigania uhuru. Rais wa kwanza wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta, akatuanzisha vibaya kwa kutushindilia katika mfumo wa kinyama wa ubepari. Badala ya sera za kuhakikisha ardhi na rasilimali za kitaifa zinatumika kwa ajili ya maendeleo ya kunufaisha na kuinua kila mtu katika jamii na kila sehemu ya Kenya, akachagua sera za kufanya rasilimali za kitaifa kumfaidi yeye binafsi, jamaa yake, marafiki zake na watu wachache huku akibagua sehemu zingine za nchi. Badala ya kujenga taifa lenye msingi katika mfumo wa ujima uliyokuwa sehemu ya utamaduni wa makabila mengi ya Kenya, Kenyatta akatutumbikiza katika mfumo wa kushindana, kunyang’anyana, kuporana, kunyakua, kunyonyana, kudanganyana na kudhulumiana.
Badala ya kukuza mbegu za kidemokrasi, haki za binadamu, umoja wa kitaifa na kuheshimu utu wa kila mtu, akapanda mbegu za imla, nyanyaso, uvunjaji haki za binadamu na uhasama kati ya makabila ndugu ya nchi yetu. Badala ya kufundishwa kuzingatia haki na usawa, Wakenya wakaelekezwa kuabudu pesa, ulafi na kutumia madaraka kujitajirisha kwa ufisadi na wizi wa mali ya umma. Badala ya kuimarisha Jumuia ya Afrika Mashariki, Serikali ya Kenyatta ikaihujumu na kuivunja kwa hofu ya siasa za ujamaa za Mwasisi wa Taifa la Tanziania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Chini ya mfumo wa ubepari, watu wachache wakazidi kutajirika huku wengi wakididimia kwenye lindi la ufukara, ukosefu na dhiki za kila aina. Serikali zote zilizofuata, iwe ni ya Daniel Arap Moi, Mwai Kibaki na hii ya leo ya Mwai Kibaki na Raila Odinga, ziliamua kufuata nyayo za kibepari za Jomo Kenyatta. Hivi leo Kenya imetia fora katika kutekeleza sera za kibepari na kukua kwa pengo kati ya matajiri na maskini.
Umma wa Kenya ulipogundua kuwa viongozi hawakuwa na nia ya kuleta ukombozi wa kijamii na kitaifa bali shauku ya kujinyakulia na kujilimbikizia pesa, ardhi na mali kwa njia yoyote ile, ulianza kuwachukia na kuwadharau. Siku Kuu za Kitaifa zikaanza kukosewa faida na kususiwa. Maana hotuba za viongozi zilijaa uongo, utapeli na unafiki. Hivi leo ni watu wachache mno ambao huhudhuria sherehe hizi. Na wanaohudhuria huhudhuria siyo kusikiliza hotuba ya Rais bali kuona michezo na kushuhudia vituko mbalimbali. Isitoshe, badala ya sherehe za kitaifa kuleta furaha zinaleta hofu na wasiwasi miongoni mwa viongozi wanaoogopa aibu ya kuzomewa na umma wenye chuki na hasira. Wananchi kwa upande wao wanaogopa athari za maandamano ya wakereketwa wanaozatiti umma kudai mageuzi nyakati za sherehe zenyewe. Uongozi mbaya umekojolea hisia za kizalendo miongoni mwa umma na kusababisha ghadhabu, hamaki na kiherehere.
Hali ya hatari ya kiuchumi na kifedha ya ubepari wa kimataifa imeongeza tabu juu ya tabu miongoni mwa umma wa Kenya huku ikizidi kuchochea mizozo na ghasia zilizoko. Wala maisha ya wengi nchini hayataboreka chini ya mfumo wa unyonyaji wa mtu kwa mtu, ubepari. Matamshi ya Serikali ya Rais Mwai Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga kuhusu haki, usawa, demokrasi, uhuru, uzalendo, utawala mwema, maadili ya kiutu, haki za binadamu na matumaini huku wakishikilia na kutekeleza sera za kibepari, ni unafiki, uhange na utapeli mtupu. Chuki zilizoko dhidi Serikali na viongozi ni chuki dhidi ya maisha duni kwa wengi miaka arobaini na sita chini ya mfumo wa ubepari. Na kadiri uchumi utakavyozidi kuyumba na kuzorota huku viongozi wakitekeleza sera za kibepari zilizofeli kwa ajili ya maslahi yao ya ulafi, watazidi kuchukiwa na umma. Ndiyo, umma unazidi kufahamu kwamba hawataona uhuru kamili ndani ya mfumo wa ubepari wala hawatakombolewa na wenye kuzingatia itikadi ya kibepari, wawe wazee wawe vijana, wanawake au wanaume. Ukweli na usemwe, barabara ya ukombozi kamili ni ya usoshalisti.
Mwandawiro Mghanga, Barua pepe: mwandawiro2002@yahoo.com
Naunga mkono mawazo yako. Endapo viongozi wetu wangefikiria kwa mkondo huu basi wakenya wangeisahau na kuizika ubepari kwenye kaburi la sahau. Heko na hongera kwa kuyaweka wazi uongozi wa kiimla unaendelezwa na viongozi amboa sisi ndio tunawachagua kwa kutuhadaa kwa maneno matamu tukiwa na matumaini ya kuboreshwa kwa maisha yetu.sisi kama wakenya wazalendo tuungane pamoja ili tukemee ubepari(pepo mbaya)
Waama, twahitaji ukombozi nchini mwetu. Swali ni je tutaupataje?