Makala ya Nguvu ya Hoja kwa Taifa Jumapili Mei 2, 2010
na Ndugu Mwandawiro Mghanga

Katika kura za maamuzi kuhusu katiba mpya ya kitaifa zitakazofanyika hivi pindi mwakani, nitapiga kura ya ndiyo ya kufanya rasimu ya katiba iwe katiba mpya ya Kenya. Huu pia ndiyo msimamo wa Social Democratic Party of Kenya (SDP). Aidha, ninawaomba wasomaji wote wa makala haya wajiandikishe kwa wingi kuwa wapigaji kura ili wawe tayari kupiga kura ya ndiyo wakati wa kura ya maamuzi itakayoamua hatima ya harakati za kuwania katiba mpya. Kwa sasa sote tuendelee kuwa wakereketwa wa kuipigia debe rasimu ya katiba. Maana sababu za kusema ndiyo kwa rasimu ya katiba tunazo. Nitataja chache tu.
Wakenya wengi tunataka na tunahitaji katiba mpya ya kitaifa. Kila hatua tuliyoipiga mbele kuelekea kwa katiba mpya imetokana na mapambano makali ambayo yaliwalazimu wazalendo kukamatwa, kuteswa, kufungwa, kukimbizwa uhamishoni na hata kuuawa. Inasikitisha kuwa Rais mstaafu Daniel Arap Moi na wafuasi wake ambao walikuwa wakipinga demokrasi na katiba bado wanaendelea kufanya hivyo leo. Wanaipinga katiba kutokana na sababu za kulinda masilahi yao ya kibinafsi ambayo ni ya kupinga ya wengi. Tumeipigania katiba kwa muda mrefu mno. Na kila ikikaribia huwa tunashindwa kuipata kwa sababu moja ama nyingine. Ndiyo kwa maana sasa lazima tuipate kwa vyovyote vile. Na kuna matumaini maana wakati huu pia Rais na Waziri Mkuu wameungana kuiunga mkono rasimu ya katiba.
Rasimu ya katiba kwa ujumla inamulika maoni ya watu wote wa Kenya wa makabila na sehemu mbalimbali yaliyokusanywa na tume ya urekebishaji katiba iliyokuwa imeongozwa na Yash Pai Ghai na vilevile kamati ya wataalamu chini ya uwenyekiti wa Nzamba Kitonga. Ndiyo kwa maana tukiichambua hii rasimu tunaona inatuunganisha zaidi kama taifa la Kenya.
Ndiyo, rasimu ya katiba ina dosari zake, ela hatuwezi kuwa na katiba ya umalaika ama ambayo inatosheleza maoni ya kila mtu. Maana katiba hutokana na mwafaka, na katika kuleta mwafaka huwezi kulazimisha wengine kukubaliana na mambo yako yote. Mwafaka huhusu kupata mengine na kupoteza mengine. Ndiyo ninashindwa kuelewa na msimamo wa baadhi ya viongozi wa kanisa ambao wanataka kulazimisha Wakenya wote kukubaliana na msimamo wao kuhusu katiba. Kwa bahati nzuri ni Wakiristo wachache watakaokubaliana na msimamo huu wa kuvuruga mwafaka wa Wakenya kuhusu katiba.
Aidha, dosari zilizoko katika katiba hazitoshi kutuzuia kuwa na katiba mpya. Tena ukweli kuhusu katiba utajulikana katika utekelezaji wake. Kwani wakati tutakapoanza kuitekeleza katiba mpya ndipo tutafahamu ukweli wote kuihusu. Yale mengi mazuri yaliyoko katika rasimu ya katiba yatakubalika na kukua sehemu ya utamaduni wa nchi yetu. Yale tutakayoyapata hayafai tutayachuja, kuyachekecha na kuyatupilia mbali ili tuendelee kuiboresha katiba kutosheleza masilahi yetu ya kitaifa.
Isitoshe, katiba si Bibilia au Korani takatifu ambazo haziwezi kurekebishwa milele. Katiba tumeitengeneza sisi wenyewe na tutairekebisha kila inapohitajika kufanya hivyo. Na madhali maendeleo ni mabadiliko ya kusonga mbele na kuboresha hali na maisha, basi katiba nayo itakuwa katika mkondo wa maendeleo. Hivyo basi itabidi ibadilike kufungamana na hali halisi na maendeleo. Wala tusiseme tunafanya katiba kwa vizazi vya sasa na vijavyo. La hasha, tunafanya katiba kwa ajili ya vizazi vya sasa. Vizazi vijavyo vitakuwa na hali zao, mambo yao na mahitaji yao ambayo yatahitaji katiba zao nyakati zao. Kile kitakachowafaa katika katiba yetu wakati wao ndicho watakachokirithi. Mengine yatawekwa katika kumbukumbu za kihistoria.
Hatima ya mambo yote yanayofanya katiba, yawe ni kuhusu uraia, mfumo wa utawala, ardhi na maliasili, mazingira, uchumi, fedha, sheria, utamaduni, na kadhalika, ni haki za binadamu. Katika rasimu ya katiba haki za binadamu zimefafanuliwa kwa marefu na mapana na kupewa uhalisi katika haki za kijamii na kiuchumi kama haki ya chakula, nyumba, maji, mazingira masafi, elimu, matibabu, msaada kwa wanyonge, na kadhalika. Kusema kweli, orodha ya haki za binadamu katika rasimu ya katiba ni mojawapo bora na za undani zaidi ulimwenguni kote. Bila shaka changamoto itakuwa katika utekelezaji wake na hili ni swala la siasa na harakati za kitabaka.
Ndiyo kwa maana tunakariri kila mara katika makala haya kuwa tujisajili kuwa wapigaji kura na tuwe tayari kupiga kura vizuri kwachagua viongozi wazuri ambao watatumia mamlaka tutakayowapa kuitafsiri na kuitekeleza katiba mpya kuboresha maisha ya kila mtu. Tukiwachagua majangili kuwa viongozi kwa misingi ya ukabila, hongo na kutojali hakika katiba mpya haitafaa thumni bali itakuwa kilemba cha ukoka kwa wengi.
Mwisho, sababu zinazotolewa na viongozi wachache wa kanisa hazifai kabisa kutunyima katiba mwaka huu. Kama ni kuweko kwa mahakama ya kadhi katika rasimu ya katiba yako katika katiba ya sasa na hata tukikosa katiba mpya yataendelea kuwako.
Hatujakuwa na mizozo ya kidini Kenya, mbona tutibue mambo na kuanzisha mizozo kati ya Wakiristo na Waisilamu kwa kuwanyanyasa ndugu zetu Waislamu? Wala katiba haijasema kuwe na uavyaji mimba wa kiholela. Ilivyopo ni kuwa bunge na wananchi watajadiliana kuhusu hali ambapo uavyaji mimba utahalalishwa maadamu kuna hali inayomlazimisha mwanamke kuavya mimba kimakusuudi. Rasimu ya katiba inafaa, tuipigie kura iwe katiba mpya ya kitaifa mwaka huu huu.
Mwandawiro Mghanga, Barua pepe: mwandawiro2002(at)yahoo.com