Ukweli wa Mambo: Mabadiliko ya Hali ya Hewa…

MABADILIKO YA HALI YA HEWA – SWALA NYETI LINALOKABILI ULIMWENGU

Makala ya Nguvu ya Hoja kwa KSB Jumamosi Disemba 12, 2009
na Ndugu Mwandawiro Mghanga

Ndugu Mwandawiro Mghanga

Mabadiliko ya hali ya hewa ni swala nyeti, siyo tu nchini, bali pia ulimwenguni kote. Maana hivi sasa ni bayana kuwa binadamu akiendelea na mtindo wa maisha ya ubepari, ya kutumia maliasili kiholela ili kuzalisha faida kwa watu wachache pasina kujali masilahi ya wengi na mazingira, dunia itahiliki hatimaye. Hivyo basi, lazima tunaoishi leo popote tulipo ulimwenguni tuwajibike kwa vizazi vya leo na kesho.

Ni katika hali hii ambapo Kenya imepeleka ujumbe mkubwa na wa hali ya juu unaoongozwa na Rais Mwai Kibaki, katika Kongamano la kimataifa kuhusu mazingira linaloendelea huko Kopenhagen, Denmark. Inatia moyo kwamba ujumbe wa Kenya wa serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali unashirikiana na nchi zingine za Kiafrika na zile zinazoendelea kudai fidia kutoka kwa nchi za viwanda na kibepari kama Marekani, Ulaya, Japan, Canada, Urusi na China. Hivi ndivyo inavyopaswa kuwa. Kwani nchi za kibepari ndizo zinazotumia maliasili zaidi na kuharibu mazingira ya ulimwengu zaidi kwa kuzidisha joto angaani kupita kiasi na hapo kusababisha athari mbaya kwa hali ya hewa angani.

Watasema na kuamua jinsi wanavyoamua huko Denmark, ila ukweli wa mambo ni kwamba Ili kuhifadhi uhai ulimwenguni, mfumo wa ubepari unaofuja maliasili na kujenga maadili ya kutumia rasilimali kiholela na kwa ulafi na kwa ajili ya watu wachache tu, lazima ukomeshwe. Mitumba ya nguo na bidhaa tilatila za viwanda inayotiririka kutoka nchi za Magharibi hadi za Kusini kama Kenya, ni dhihirisho la mtindo maisha wa kuponda mali kufa kwaja ambao ni utamaduni wa nchi za kibepari, lakini ambao unaharibu mazingira, kuzidisha joto angani huku ukifuja maliasili na maumbile.

Nchi Kaskazini, pamoja na Uchina, zinabugia malighafi kutoka nchi za Kusuni kama Afrika kwa ajili ya viwanda vyao. Wakati huohuo nchi za Kusini zinashindiliwa bidhaa za viwanda kutoka Kaskazini. Isitoshe, nyingi ya bidhaa hizo ni mitumba, si za umuhimu wala hazihitajiki na idadi kubwa ya watu wa nchi Kusuni. Tena zinazidisha uharibifu wa mazingira. Ndiyo kwa maana, ili Kongamano la Denmark lifaulu, sharti nchi za Kaskazini na Uchina ziwajibike, lazima zifidie nchi za Kusini zinazoathirika vibaya zaidi kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa yanayochangiwa maendeleo ya kibepari kaskazini na Uchina. Fauka ya haya, lazima nchi za Kaskazini na Uchina zifanye ahadi za kweli za utekelezaji wa mikakati halisi ya kupunguza viwango vyao vya kuongeza joto angani.

Tayari athari za mabadiliko la hali ya hewa zimeathiri vibaya kila sehemu na jamii Kenya: mvua haijanyesha jinsi ilivyokuwa imetabiriwa na wataalamu wa hali ya hewa; kilimo kinafeli kwa kuzidi kwa ukame; maelfu ya mifugo imekufa kwa kukosa malisho na maji na jamii za wafugaji sasa zinadorora kwa kukosa lishe, dhiki na ufukara; njaa bado inayoendelea nchini bado ni mtikisiko wa kitaifa; chemichemi za maji zinapotea huku mito ikikauka; wanyamapori pia wanakufa kwa njaa na kiu; vita kati ya binadamu na wanyamapori vimeongezeka; usalama unazoroteka huku vita vya kikabila vya kuibiana mifugo na kushindania maliasili vikiongezeka; umeme umepungua na kughalika; ufukara unakua kila siku miongoni mwa umma; uhalifu unazidi; uchumi unayumba na kukwama.

Ndiyo kwa maana hatutasita kukariri: mabadiliko ya hali ya hewa ni mtikisiko wa kitaifa, ni hali ya hatari, ni swala la kufa na kupona. Ni jukumu la kila mtu popote pale alipo kujitahidi kiasi cha uwezo wake wote kuchangia uhifadhi wa mazingira. Mvua ikinyesha tupande miti; tuhifadhi chemichemi za maji na sehemu za unyevunyevu; tulinde mito na maziwa yetu; tulime huku tukihifadhi udongo; tulishe siyo kwa ajili ya kuwa na mifugo mingi tu ya kuonekana bali ili itusaidie na pia isiharibu mazingira; tujitayarishe kuhifadhi maji ya mvua kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na kilimo; tuzidishe juhudi za kupanda mimea ya chakula huku pia tukifufua ile ya kienyeji na tupeane mwamko wa uhifadhi wa udongo. Tuishi maisha bora lakini rahisi.

Tusiponde maisha wala kutumia bila kujali au kuhifadhi. Tukatae mfumo wa ubepari na mtindo wake wa maisha. Aidha, tuanze kujiuliza: je, ni lazima tuzikane kwa majeneza ya mbao? Ni misitu ngapi inayokatwa kila siku ili kutengeneza majeneza? Tunawezaje kuhifadhi misitu huku tukikata maelfu ya ekari za miti nchini ili tu kuzizika na maiti chini ya mchanga kila siku? Hakika tunaweza kuzikana kwa heshima na kiutu bila majeneza ya mbao.
Mwisho, inasikitisha sana kuwa Serikali ya PNU na ODM iliyoko inaendelea kuwa kikwazo cha uhifadhi wa mazingira. Bado inasitasita katika kutekeleza sera ya kuhifadhi Msitu wa Mau na misitu mingine nchini. Sera ya kitaifa ya ardhi itakayosadia matumizi ya haki ya ardhi inayoambatana na uhufadhi wa mazingira bado ni ahadi tupu kutoka kwa serikali hii. Inaonekana kuwa viongozi hawana haja ya kulinda uhai wa nchi bali kuhifadhi viti vyao vya uongozi kutumia siasa duni za kujipendekeza. Ili kuhifadhi mazingira na kuokoa nchi lazima tufanye mageuzi.

Mnamo mwaka wa 2012 tuwafanye wawe viongozi wazalendo wanaojali masilahi ya kitaifa na ya binadamu wote. Maana bila kuwa na uongozi wa kutekeleza sera za haki, usawa na usimamizi bora wa maliasili kwa manufaa ya kila wa mtu wa kizazi cha sasa na chijacho, tutaangamia hatimaye kama taifa na kama binadamu. Fauka ya haya pia tutaangamiza viumbe vingine na uhai duniani.

Mwandawiro Mghanga, Barua pepe: mwandawiro2002(at)yahoo.com

One comment

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.