MAADA: BEI ZA BIDHAA ZA CHAKULA KWA WANANCHI WA KAWAIDA:
Maandamano 31. Mei 2011
Maada: Bei za chakula kwa wananchi wa kawaida
Je, serikali inasikiliza kilio cha makabwela?

Mfumuko wa bei za bidhaa mkiwemo chakula, nishati hasa mafuta ya taa na makaa, kodi ya nyumba na bei ya usafiri hasa ya matatu hivi sasa ni mtikisiko ambao utatikisa serikali na taifa hivi karibuni ikiwa haitatambua ukweli huu na kuchukua hatua madhubuti za kuleta ufumbuzi mara moja. Mamilioni ya Wakenya kote nchini hawali wakashiba, wanakabiliwa na baa la njaa na kuongezeka kwa dhiki za kila aina. Tayari watu wamekufa kwa njaa nchini. Hili linasikitisha. Tena linaaibisha. Na kisha linakasirisha. Aidha, linahofisha kwani bei ya UNGA wa mahindi – chakula cha makabwela – imepanda mno na kuwafanya umma kote nchini – hasa katika mitaa ya mabanda mijini – kutokota na kuchemka hasira na ghamidha za kudai mapinduzi. Je, serikali inasikiliza kilio cha umma kinachosikika kila sehemu usiku na mchana? Au inashikilia ni kelele za chura zisizomzuia ng’ombe kunywa maji!?
Tatizo la njaa halikuzuka leo – limekuwa na mafukara siku zote!
Isitoshe, sehemu nyingi nchini zimegeuka nchi kame kutokana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa yaliyosababishwa na maumbile na pia binadamu wenyewe. Tunakubali, bei ya mafuta ya nishati imepanda sana na Kenya haizalishi mafuta ya nishati. Na kupanda kwa bei ya mafuta ya nishati kunaathiri mfumuko wa bei za bidhaa. Pamoja na hayo hii si sababu ya kufanya serikali ikose kufanya na kutekeleza mikakati halisi ya kudhibiti mfumuko wa bei za bidhaa, hasa mahitaji muhimu, hasa chakula na mafuta ya taa. Isijifanye kana kwamba tatizo la chakula limezuka ghafla bin vu. Ukweli ni kwamba njaa imekuwa nasi wakati wote. Ni watu wachache tu nchini ambao wana lishe bora na ya kutosha kila mara. Ingawa tatizo la njaa limezidi leo, kwa kweli si lipya katika mitaa ya mabanda mijini, watu wa jamii za wachungaji na sehemu kame za nchi. Maskwata, wakimbizi ndani ya nchi, wachuuzi, wafanyikazi na wakulima makabwela, mara nyingi hawali wakashiba, sembuse lishe bora.
Serikali lazima iwajibike: itekeleze sera za maksuudi za kuondoa njaa nchini!
Wala tusiambiwe kuwa serikali PNU na ODM haina uwezo wa kusuluhisha tatizo la njaa. Kama haiwezi basi haina sababu ya kuwa uongozini. Nia ya kuleta suluhu endelezi ndiyo haipo maana penye nia hapakosekani njia. Kuna ukosefu wa sera halisi na za maksuudi zinazolenga kutatua matatizo ya makabwela, mkiwemo ukosefu wa lishe bora na ya kutosha. Aidha, sababu za kimsingi za njaa kwa wengi zinajulikana. Sera mbaya za kilimo na mfumo wa kibepari wa umilikaji na utumiaji ardhi zimechangia kuleta ukosefu wa lishe bora na ya kutosha kwa wengi.
Sababu za ukosefu wa chakula na njaa ni uzembe wa serikali!
Kilimo cha wakulima wadogo cha kuzalisha chakula kimepuuzwa huku kile cha mazao ya kuuza hasa – nchi za nje – kikizingatiwa na kuchukua ardhi kubwa na bora zaidi kila siku. Mathalani, ardhi kubwa kupita kiasi yenye rotuba ya mikoa ya Nyanza na Magharibi imepandwa miwa huku kilimo cha chakula kikizoroteka. Hakuna mikakati mizuri ya kufanya maghala ya kuhifadhi chakula wakati wa mavuno mazuri. Sehemu kubwa zaidi ya chakula kinaharibika wakati wa kuvuna na kikisha vunwa. Wataalamu wa kusambaza pembejeo na tekinolojia za kilimo bora kwa wakulima makabwela wamepunguzwa kutokana na shinikizo kutoka nje ya nchi. Hili limeathiri vibaya uzalishaji na kuzidisha mmomonyoko wa udongo na uharibifu wa ardhi na mazingira. Huku tukishuhudia athari za mabadiliko ya hali ya hewa, kilimo cha nchi hii bado kinaendelea kutegemea mvua ya majira huku kilimo cha unyunyizaji kikikua polepole mno na sehemu chache tu nchini. Maonyo ya awali kuhusu hali ya hewa na chakula hayatiliwi manani. Hadi matatizo yafikie mtikisiko ndipo serikali ilazimike kutangaza suluhu za kizimamoto ambazo mara nyingi ni za kuwavisha umma vilemba vya ukoka.
Njaa ni dhihirisho la makinzano ya kitabaka nchini!
Pamoja na haya yote, tatizo la njaa ni sehemu ya makinzano ya kitabaka. Njaa ni tatizo la maskini na umaskini. Si tatizo la matajiri na utajiri. Viongozi wetu na jamaa zao wanakula na kushiba. Wengi wao hawajawahi kukumbana na njaa tangu wazaliwe. Chakula kipo masokoni mijini na mashambani, bali kutokana na ufukara na mfumuko wa bei wengi hawana pesa za kukinunua. Chakula kinaoza sokoni na katika madukamakuu kwa kukosa wanunuzi huku wengi wakikitamani na kukililia. Mbwa wanakula na kusaza huku mafukara wanaramba masahani. Hii ndiyo hali halisi ya mfumo wa ubepari nchini. Ndiyo kwa maana viongozi wamekuwa wakipuuza tatizo hili ambalo limekuwako nasi siku zote. Wakati ambapo idadi kubwa ya Wakenya – ikiwa ni pamoja na maskwata na wakimbizi wa ndani ya nchi – wanalilia ardhi ya kujenga makao, kulima na kuzalisha chakula, ardhi kubwa inayomilikiwa na kuhodhiwa na jamaa chache za kibwanyenye hailimwi wala haitumiki kwa uzalishaji na maendeleo yoyote.
Utekelezaji wa sera za kibeberu nchini unavuruga uchumi na kusababisha njaa!
Uchumi wa biashara, viwanda na kilimo wa kitaifa umeathiriwa vibaya mno na sera za utandawazi wa kibeberu wa uhuruishaji na ubinafsishaji wa uchumi na maisha zinazotekelezwa na serikali ya PNU na ODM. Hili limesababisha ukosefu wa ajira ambao unawafanya Wakenya wengi kuzidi kuwa wachuuzi wa mitumba na bidhaa duni kutoka nchi za nje. Mitumba hutengeneza uchumi wa viwanda na ajira pahali zinapotoka na kuharibu uchumi wa viwanda na ajira nchini. Sera ambazo hazilindi uchumi wa kitaifa, zinazopunguza ajira na kusukuma wengi pembeni haziwezi kutengeneza soko la ndani na kwa sababu hiyo haziwezi kuhamasisha kukua kwa uchumi wa kilimo na viwanda. Matokeo yake ni kuzidi kwa ufukara, upungufu wa chakula na hata njaa.
Badala ya kusambaziwa ’chakula cha msaada’ wahanga wapewe pesa taslimu!
Kufungamana na kifungo 43 cha Katiba ya Kenya kila mtu ana haki kuwa na mahitaji ya kimsingi mkiwemo lishe bora na ya kutosha na hali ya kuepukana na njaa. Kutokana na sera mbaya za kiuchumi, kisiasa na kijamii wananchi wengi wanakabiliwa na njaa. Basi lazima serikali itoe ruzuku ya chakula (’chakula cha msaada’) kwa wahanga wa njaa kote nchini. Ruzuku ya chakula kutoka kwa serikali si msaada bali ni haki yawahanga wa njaa. Bali ni suluhisho la muda mfupi na la kizimamoto tu. Aidha, usambazaji wa ’chakula cha msaada’ kinawadunisha wahanga wa njaa na tena ni ngome ya utapeli na ufisadi. Asilimia kubwa zaidi ya mabilioni ya pesa yanayotumika kununua na kusambaza chakula cha msaada hufaidi zaidi waagizaji wa nafaka kutoka nje; wenye malori; wafanyibiashara wachache wateule marafiki na washirika wa viongozi; walanguzi wa kila aina kutoka ngazi za juu za serikali hadi za mashinani. Kwa wahanga wa njaa, chakula cha msaada kimekuwa cha kuwapaka mafuta nyuma ya chupa. Wahanga wa njaa wapewe pesa taslimu badala ya kuwanunulia na kuwasambazia chakula ambacho si chaguo lao. Wananchi wakiwa na pesa mikononi masoko huria yataleta chakula karibu nao.
Mwisho, haki ya lishe bora na ya kutosha haiwezi kupatikana bila muungano na mapambano ya umma. Tukumbuke maandamano ya amani ni haki ya kikatiba (kifungo 37 cha Katiba ya Kenya). Tushiriki maandamano ya UNGA mnamo Jumanne Mei 31, 2011 ili tujiokoe na njaa!!!
KAMATI YA UNGA REVOLUTION
Email: ungarevolution@gmail.com
Facebook: UNGA REVOLUTUION
Tel: 0702655596
Otieno Sidi: Co Convener
Gacheke Gachihi: Bunge la Mwananchi
Mulialia Okumu: Co Convener
James Kamau: Unga Revolution Committee Mukuru
Francis Sakwa: Unga Revolution Committee Mathare
Florence Kanyi: Unga Revolution Committee
Benard Wachira: Social Democratic Party
CC. All Media Houses
The People of Kenya
ENJOY THE TRIGGER-HAPPY KWEKWE KILLER SQUAD AT IT MURDERING SUSPECTS INSTEAD OF ARRESTING THEM>http://www.nation.co.ke/News/-/1056/1172120/-/10wl9r0z/-/index.html
I cant see anybody serious among these groups of youth who can carry out or lead any revolution in Kenya hence lack of political unity ,Ideology ,solidarity ,organisation , military vanguard ,strategy ,logistic and leadership. They are just a bunch of naive youth brought up about in a Rotten Capitalism sick society based on hate ,bougueousy propaganda ,cowed and tamed with a mentality of Money worshipping and extortionism and lack of National Pride ,patriotism Nationalism and sacrificial.
KSB: A positive aspect in the stuation is that they have understood that the country needs a revolution. It is for this reason that I made an appeal to revolutionary thinkers like yourself to help advance the process. They need help in understanding what is to be done otherwise they have taken the first step. It is like trying to fly an airoplane with the knowledge of aviation. You can guess what might happen.