Makala ya Nguvu ya Hoja kwa Taifa Jumapili Mei 23, 2010
na Ndugu Mwandawiro Mghanga

Kama utaratibu wa kisheria wa kufikia hatima ya katiba inayopendekezwa ya Kenya ungelizingatiwa, hiki ni kipindi cha kuwaelimisha wananchi kuhusu kile hasa kinachapendekezwa na katiba pendekezo. Wala huu si wakati wa kampeni za KIJANI KIBICHI na NYEKUNDU. Ilivyoko sasa ni kwamba wenye kuunga mkono katiba pendekezo ni wa rangi ya KIJANI KIBICH na ambao wanaipinga rangi yao ni NYEKUNDU. Swala la kumua kutumia rangi katika kura za maamuzi kuhusu katiba zimezua hisia mbalimbali.
Kwa mfano, sisi wa siasa za mlengo wa kushoto hupendelea sana rangi nyekundu. Ndiyo kwa maana tukiona rangi nyekundu ikiwa alama ya wanaoipinga katiba pendekezo huku sisi tukiiunga mkono tunachanganyikiwa si haba. Lakini jambo la msingi ninalolisema hapa ni kuwa tayari kampeni za KIJANI KIBICHI na NYEKUNDU zimeanza hata kabla ya muda wake kufikia. Labda ni kwa sababu ya utamaduni wa Wakenya na viongozi wake wa kupuuza sheria au pengine ni kwa vile elimu yoyote ile haiwezi kutenganishwa na msimamo maalumu, uwe wa kiitikadi au wa kitabaka.
Basi maadamu elimu na kampeni za katiba mpya zinaendelea sambamba, ushauri wa makala haya ni kwamba zifanyike kwa kuzingatia ukweli, amani na uzalendo. Wakati wote tukumbuke kuwa shabaha ya kupigania katiba mpya ni kutuongezea umoja wa kitaifa, demokrasia, haki za binadamu, amani, uhuru, utawala bora na uwezo kuwa na usimamizi mzuri wa rasilimali zetu ili kufanya maendeleo endelevu ya kuhakikisha kuwa kila mtu nchini anaishi maisha anayostahili binadamu kuishi.
Tusisahau kwamba kwa vyovyote vile baada ya kura za maoni sote tutaendelea kuishi ndani ya Kenya tukiwa Wakenya. Hivyo basi, kampeni za katiba mpya ni tofali la barafu ambalo litayeyuka na kupotea baada ya tarehe 4 Agosti mwaka huu. Kwa hivyo kampeni zifanyike bila chuki, maana demokrasia huhusu hali ya kila upande kuwa na fursa ya kusema na kusikilizwa kisha uamuzi unafanywa na wapigaji kura huku kila upande ukikubali uamuzi wa wapigaji kura.
Kwa wale wenye upande wa KIJANI KIBICHI wa kupigia debe katiba inayopendekezwa ya Kenya, hatuhitaji kusema uongo, kutia chumvi au kufanya propaganda zisizo na uweli, maana kizuri chenyewe hujiiuza wakati ambapo kibaya hujitembeza. Katiba ya Kenya inayopendekezwa ni nzuri sana kwa ujumla, na kila atakayeisoma kwa makini ataona hivyo yeye mwenyewe. Tukiwaelimisha wananchi kwa kunukulu ukweli kama ulivyo katika katiba yenyewe wakati tunapowaelimisha wananchi tutafanya kampeni ya kutusaidia zaidi.
Aidha, wakati wote tusisitize kwamba hata baada ya katiba pendekezo kuwa katiba ni haki na wajibu wa kila mzalendo kuwa na katiba mkononi kila wakati ili aendelee kuisoma na kuifahamu kuweza kuitumia kutambua haki zake na majukumu yake. Hili litaambatana na taifa kuhakikisha kuwa kila Mkenya anajua kusoma na kuandika na pia kwamba katiba inatafsiriwa katika kila lugha ya Wakenya.
Wenye alama NYEKUNDU wana kibarua kikubwa cha kutoa sababu za msingi zilizoko ndani ya katiba pendekezo za kutuzuia tusipate katiba mwaka huu. Kusema kweli, mimi sioni sababu ya kimsingi ya kunifanya nisiwe upande wa KIJANI KIBICHI. Ninaona matumaini ya kuanzishwa kwa Kenya mpya na bora tutakapopata katiba mpya baada ya kuipitisha katiba inayopendekezwa kwa kura za maamuzi mnamo Agosti mwaka huu.
Si kweli kwamba katiba inayopendekezwa ya Kenya ni mradi wa serikali. Serikali ya sasa ni ya PNU na ODM. Ikiwa katiba pendekezo ni mradi wa serikali mbona viongozi wengine wa serikali hiyo hiyo wako upande wa NYEKUNDU? Chama chetu cha SDP, kwa mfano, kama vyama vingine ambavyo haviko serikalini, tunaunga mkono katiba inayopendekezwa na sisi hatuko kwa serikali leo. Isitoshe, tumeshiriki katika harakati za kupigania katiba mpya katika kila hatua na kutoka kitambo kama wazalendo wengine. Ndiyo kwa maana tunashangaa kusikia watu wengine wakidai ati katiba pendekezo ni mradi wa serikali. Tusidanganye tukatibua mambo kwa kuzua porojo zisizofaa, ukweli ni kuwa katiba inayopendekezwa ni mradi wa wazalendo na umma wa Wakenya. Katiba mpya itakuwa ya Wakenya wote na tusikubali ifanywe kuwa ya serikali iliyopo leo na itakayokuja kesho.
Tayari mabilioni ya pesa za umma yametumika katika kutufikisha hapa tulipofika katika safari ya kuelekea kwa katiba mpya. Hata sasa tume ya wataalamu kuhusu katiba imepewa pesa za umma kuendesha elimu kuhusu katiba pendekezo. Viongozi wa serikali wanaendelea kutumia pesa za umma katika kampeni za kuunga mkono katiba pendekezo. Hili hatupingi, tunachokipinga ni kujaribu kutumia pesa za umma kufadhili vyama vilivyoko katika serikali kufanya kampeni ya KIJANI KIBICHI. Kila Mkenya ana haki na wajibu wa kushiriki katika kampeni za katiba mpya na wala asifanye hivyo kwa kuwahonga watu au kutegemea kuhongwa. Katiba mpya itakuwa yetu sote na hatuwezi kuithamini ikiwa tutaitumia kuchuma pesa za umma na wafadhili.
Wafadhili wamemwaga pesa nyingi za kuipigania katiba inayopendekezwa ya Wakenya. Wenyewe wafadhili kutoka nje wameichukua katiba mpya kama mradi wao pia. Nina hofu. Ukiona mgeni katika matanga akilia kuliko waliyofiwa wenyewe tahadhari huenda kuna jambo. Tukitegemea kusaidiwa kwa kila jambo, hata katiba ya kitaifa, tutasakamwa na kukosa uhuru. Tuipitishe katiba mpya itukombowe na kutuongezea uhuru wa kitaifa, tusibaki pale pale!
Mwandawiro Mghanga, Barua pepe: mwandawiro2002(a)yahoo.com