Makala ya Nguvu ya Hoja, KSB Jumapili Machi 7, 2010
na Ndugu Mwandawiro Mghanga

Matokeo ya mtihani wa kidato cha nne yalitangazwa Jumatano juma hili na Waziri wa Elimu Profesa Ongeri. Matokeo haya ni muhimu kwani yanaamua kwa kiasi kikubwa hatima ya mwelekeo wa elimu wa wanafunzi wanaohusika.
Tulitazama katika runinga shule zilezoongoza katika mtihani wa mwaka huu zikisherehekea kwa vifijo na nderemo. Aidha tulishuhudia wanafunzi waliyokuwa katika mstari wa mbele wa kuhitimu vizuri zaidi wakibebwa na wanafunzi wanzao ambao wanajivunia ufanisi wao. Wao wenyewe walijawa tabasamu midomoni na bila shaka walimu na wazazi wao wanawaonea fahari. Makala haya yanachukua fursa hii kuwapongeza wanafunzi wote ambao kutokana na bidii na nidhamu wamefaulu kufanya vizuri katika ngazi hii ya kutafuta na kuelekea kwa elimu ya juu. Vilevile, tunawahongera walimu na wazazi ambao bila shaka wana sehemu kubwa katika kilicholeta ufanisi ya wanafunzi wao. Ni muhimu ari ya kupigania matokeo bora ya kila jambo itambuliwe na kupewa kipaumbele.
Pamoja na hayo, matokeo ya mtihani huleta huzuni kwa wengi kila wakati. Wanafunzi ambao hawakupata matokeo mema huhuzunika pamoja na wazazi wao, walimu wao na shule zao. Na kuna wale ambao huadhibiwa kwa kunyimwa matokeo kwa sababu za kudanganya katika mtihani, ziwe ni za kweli au ni za uongo. Kwa wale ambao hawakuhitumu vizuri tunasema matokeo mabaya ya mtihani yasiyo mwisho ya kutafuta elimu. Kwani kuvunjika kwa kalamu si mwisho wa kuandika.
Mimi pia huwa na huzuni kila ninaposikia matokeo yakitangazwa na kuangaziwa na vyombo vya habari. Lakini sababu ya huzuni yangu ni tofauti na tena ni nyeti. Mimi husikitika kwa kuhisi kuwa matangazo ya matokeo ya mtihani hutumika kuwakejeli watoto wa mafukara pamoja na wazazi wao na makabwela wengi kwa ujumla. Vilevile hizo mbwembwe zinazoambatana na matangazo ya matokeo ya mitihani zinatumika kuwacheka na kuwatemea mate watoto wengi waliyowekwa pembeni ni mfumo wa kijamii – kiuchumi unapendelea, kujenga na kuendeleza wachache huku ukiwapuuza, kuwachuja, kuwachekecha na kuwatupa wengi.
Mfumo wa kijamii – kiuchumi wa Kenya leo ni wa kitabaka, wa mwenye nguvu mpishe mnyonge msonge. Ni mfumo wa kung’angana, kunyang’anyana, kudanganyana na kushindana kama wanyamapori. Katika hali hii maadili ya huruma na kusaidiana yamewekwa kando huko yale ya ulafi na ubinafsi yakizingatiwa. Nao mfumo wa elimu unamulika maisha halisi ya nchi yetu ya ubepari. Badala ya elimu kutumiwa kuleta usawa katika jamii inatumika kuzidisha utabaka, inatumiwa kuongeza pengo kati ya matajiri na maskini. Kwani kuna shule za kibinafsi na za umma. Katika shule za kibinafsi kuna zile za hali ya juu zenye mazingira ya bora kwa kila hali ya kupeana elimu na zile za kawaida lakini bora kuliko za umma. Shule nyingi nchini ni za umma nazo zinatofautiana kwa kila hali katika hali ya utaoji elimu. Kuna shule nzuri za umma lakini nyingi, hasa katika sehemu kame na mbali na katika mitaa ya mabanda ni bovu. Lakini mtihani ni ule ule tu.
Si ajabu kwamba ni shule zilezile tu ambazo huwa mbele kila mwaka. Nazo ni zile zenye vifaa bora zaidi vya elimu na ambazo wenye uwezo wa kipesa hupeleka watoto wao. Hakuna haki wala usawa katika mashindano lakini washindi hutangazwa na kusifiwa huku waliyoshindwa katika mfumo wa elimu usiyo na haki huchekwa na kubezwa na viongozi na vyombo vya habari. Ilivyoko sasa ukiwa na pesa mtoto wako atapata elimu nzuri zaidi na fursa bora zaidi ya kuendelea mbele katika maisha. Usipokuwa na pesa shauri yako na watoto wako! Hakika hatuwezi kujenga nchi yenye amani, usalama, demokrasi na maendeleo endelevu kwa kutumia mfumo wa elimu unaoendeleza utamaduni wa kuwarudisha na kuwawacha wengi nyuma.
Aidha, siyo tu mfumo wa elimu Kenya ni wa kibaguzi, bali ni mfumo ambao haujengi maadili ya kiutu ya kuhurumiana, kusaidiana na kuendelezana miongoni mwa wanafunzi. Wanafunzi darasani wanafanywa kushindana kati yao badala ya kusaidiana katika masomo. Wale wenye uwezo zaidi hawafundishwi kutumia uwezo wao kuwapa wenzao uwezo kama wao bali ili kuwashinda na kuwa mbele zao. Badala ya kuwapa watoto elimu ya kuwafanya watambue na kuendeleza vipawa vyao tunatumia wakati mwingi zaidi katika kuwafanya wapite mitihani tu. Kwa ufupi, badala ya kuzingatia elimu tunazingatia mitihani katika shule zetu. Mfumo wa elimu kutathmini vipawa vya watoto kwa mitihani ya siku chache katika historia ndefu ya masomo haufai. Tena ni mbaya zaidi katika hali ambapo hakuna usawa wa mazingira ya masomo na huku mtihani ni mmoja. Hivyo basi tunadai mfumo wa elimu wa usawa na wa kujenga binadamu anaetambua ubinadamu wake na mwenye ujuzi kuchangia maendeleo ya taifa unaotokana na kuendelezwa kwa vipawa alivyozaliwa nazvyo.
Mwandawiro Mghanga, Barua pepe: mwandawiro2002@yahoo.com