Makala ya Nguvu ya Hoja, KSB Januari 27, 2012

Maendeleo ni kuongezeka kwa kuboreka kwa hali na maisha katika jamii. Maendeleo endelevu ni yale yanayohusisha, kunufaisha na kuendeleza watu wote katika jamii bila kuwacha wengine nyuma na pembeni. Ni kuhakikisha kuna usawa wa kijinsia na pia kutambuliwa na kuendelezwa kwa lugha na tamaduni za makabila yote yanayoishi nchini. Ni pamoja na kutumia vizuri, kulinda na kuhifadhi maliasili na mazingira. Ni kujenga utamadini wa demokrasi, amani, usalama na haki za binadamu ili kufanya maendeleo yanayokua na kujiendeleza kadiri wakati unavyoendelea. Ni kuondoa ufukara kwa wote.
Kenya bado hatufanyi maendeleo endelevu maana wachache tu ndiyo wanaoishi maisha bora huku wengi wakididimia katika hali ya ufukara, ujinga na ukosefu wa kila hali. Wachache wanaishi katika mitaa mizuri na ya kupendeza katika nyumba kubwa za fahari zilizozungukwa na mazingira mazuri ya mandhari ya kupendeza na ya afya. Wengi wanaishi katika mitaa ya mabanda yenye ufukara, uchafu, hatari, ghasia, uhalifu, uvundo na dhiki tilatila. Kenya ni ya mfumo wa kitabaka. Idadi kubwa zaidi ya wananchi ni wa tabaka la mafukara ambao wamenyimwa uwezo wa kushiriki katika maendeleo ya kuboresha maisha. Hapawezi kuwa na maendeleo endelevu katika hali ambapo idadi kubwa zaidi ya watu katika jamii ni mafukara ambao hawawezi kumudu mahitaji ya kimsingi chakula, nguo, nyumba, matibabu, elimu, maji na mazingira bora.
Pengo kati ya matajiri na mafukara ni kubwa mno na linazidi kupanuka kila siku. Kwani ubinafsishaji na uhuruishaji wa uchumi, ardhi na maliasili na hata na elimu na matibabu, yote haya yanawawezesha wachache tu katika jamii wenye ushawishi wa kisiasa, kiuchumi na kikoo kuendelea kutumia jasho la wengi kujilimbikizia utajiri kila siku ilihali wengi hawana fursa wala matumaini ya kujikokota kujitoa kutoka katika hali ya shida na umaskini. Watu wengi wanalazimika kuishi maisha yasiyo tofauti na ya wanyama ya kutafuta mahitaji ya kimsingi tu kila siku miaka nenda rudi, hasa chakula, bila kuwa na wakati wa kupumzika au kustarehe wala hali ya kufurahia sanaa na tamasha za kitamaduni.
Ufisadi miongoni mwa viongozi umekuwa sehemu ya utamaduni na kizingiti kikubwa cha maendeleo. Badala ya kuhakikisha sheria zinafanya kazi ipasavyo kuhakikisha usimamizi bora wa maendeleo, viongozi wanavunja na kusababisha kuvunjwa kwa sheria kiholela. Ndiyo kwa sababu barabara hazijengeki ipasavyo; mitaa ya mabanda yenye nyumba mbaya, chafu na zinazohatarisha maisha inaonekana kila pahali nchini; kiwango cha elimu ikiwemo ya juu na hasa ya chuo kikuu kimeshuka mno; uharibifu wa mazingira unaendelea; na huduma muhimu mbalimbali zinazoroteka au kukosekana huku uhalifu ukiongezeka.
Sera za kujenga na kubomoa haziwezi kuleta maendeleo. Kwa sababu ya ufisadi, ulafi, ujinga, umaskini, kutojali, kutokuwa na haya wala aibu, kutotekeleza sheria na mipango, kukubali maisha yasiyo ya kiutu, tunajenga na kubomoa taasisi badala ya kuzirekebisha, kuzikuza na kuziendeleza. Tunajenga majumba ambayo tunajua kutoka mwanzo yatabomolewa punde si punde maana yamejengwa vibaya na kinyume cha kanuni zilizowekwa. Mitaa ya mabanda ambayo itabomolewa siku zijazo inachipuka kote mijini huku wizara na idara zinazohusika zikiangalia. Hatujengi vitu vya kudumu, tunajenga vya kuharibika na kuharibiwa kesho. Hatujazoea kukarabati bali tunangojea mambo, mkiwemo barabara, nyumba na miundo msingi, yaharibike kabisa ndipo tuanze kujenga upya tena. Badala ya kuziba ufa tunangoja hadi tutakapolazimika kujenga kuta hatimaye. Ndipo pamoja na chaguzi za kila baada ya miaka mitano tunabaki palepale, hatusongi mbele. Tumeshindwa kutumia mapinduzi ya sayansi na tekinolojia yanayoendelea ulimwenguni kutoa nchi yetu kutoka kwa hali ya ufukara na kukwama na kuipeleka katika barabara ya maendeleo endelezi. Tumebaki katika hali ya kuishi maisha ya bahati na sibu na kutegemea misaada na maumbile kama wanyama.
Jambo la kusikitisha zaidi ni kuwa tunajua na kufahamu kuwa chimbuko cha kutokuwa na maendeleo endelevu ni mfumo na utawala mbaya ambao umeendesha nchi yetu kutoka wakati wa ukoloni hadi sasa. Viongozi waliyoko ni matapeli wa kisiasa ambao hawana nia wala haja ya kubadilisha hali hii kwa ubora maana wamekuwa watumwa wa maadili na vitendo vya ulafi wa kujinyakulia na kujilimbikizia kama fisi. Badala ya kupigana na umaskini wanapiga maskini. Watu ambao wametajirika kutokana na ufisadi, wizi na uporaji wa mali ya umma na hata kutokana na biashara haramu na katili ya madawa ya kulevya na kila aina ya uhalifu wanaheshimiwa na hata kufanywa viongozi. Mabilionea na mamilionea wa uhalifu wanasifiwa hata na kuombewa makanisani na misikitini. Uwoga, kutojali, unafiki, ubarakala, ukabila na mazoea ya kutegemea vya bwerere wakati wa uchaguzi – haya yote yanashindilia wengi wetu katika hali ya ufukara. Na kuongezeka kwa ufukara ni tisho kwa amani na usalama nchini. Je, tunajitayarisha kushiriki uchaguzi wa kuwachagua viongozi watakaoleta maendeleo endelevu? Au baada ya uchaguzi utakaokuja tutabaki na hali hii hii iliyoko leo? Hii ni changamoto kwa kila mwananchi, hasa wengi wanaonyonywa na kugandamizwa.
Mwandawiro Mghanga, Barua pepe: mwandawiro.mghanga(at)gmail.com
God bless u mwadawiro