Makala ya Nguvu ya Hoja kwa KSB Jumapili Aprili 25, 2010
na Ndugu Mwandawiro Mghanga

Mara nyingi nimekuwa nikijiuliza, kwa nini watu wengi hupendelea kushiriki katika mikutano ya kidini kuliko ile ya kisiasa au inayohusu mbalimbali mengine nchini? Maelfu ya watu, kwa mfano, hufurikana katika makrusedi ambayo sasa hufanyika usiku na mchana kila pahali nchini miaka nenda miaka rudi. Tena siku hizi mikutano ya maombi haingoji Jumapili, hufanyika kila wakati, asubuhi, mchana, adhuhuri, jioni na usiku. Sauti za krusedi zinasikika wakati wa kazi na wakati wa mapumziko, mijini na vijijini, hata huwa ninashangaa washiriki hupata wapi muda wa kutafuta riziki! Pamoja na hayo ukweli wa mambo ni kwamba Wakenya wanapendelea mno kushiriki katika mikutano ya kidini kuliko ya kisiasa.
Mikutano ya kisiasa huvutia watu wachache ikilinganishwa na ya kidini. Isitoshe, wanaohudhuria mikutano ya kisiasa ni walewale tu ambao ni daima ni mashabiki wa kila siku wa kisiasa, vyama vya kisiasa ama viongozi wa kisiasa. Ni walewale ambao hupigia debe viongozi wao na výama vyao kila siku. Mara nyingi vilevile ni wakereketwa wa mageuzi walewale wa siku zote. Pia maelfu ya watu ambao hawana chochote cha kufanya huhudhuria mikutano ya kisiasa kujiburudisha kutokana na hotuba za viongozi.
Si ajabu kuwa wanasiasa ambao huropoka na kupayuka chochote kinachokuja ndimini mwao pasina kuyachuja na kuyachekecha maneno yao huwa mashuhuri sana miongoni mwa wengi wanaoshiriki mikutano ya kisiasa. Wengi hushangiliwa kwa vifijo na nderemo kwa kuonyesha ujasiri na usogora wa kuwakebehi na kuwatukana viongozi wengine wa serikali na vyama. Pamoja na hayo mikutano ya kisiasa hugharimu juhudi kubwa na pesa. Kuna watu ambao huishi kwakufanya kazi ya uburoka wa kufuatana na wanasiasa ambao huwalipa kufanya kazi ya kuwahamasisha watu kuja kwa mikutano ya kisiasa. Tena wanaokuja kwa mikutano ya kisiasa wakati mwingi hushawishiwa na pesa au hutarajia pesa kutoka kwa kushiriki katika mikutano ya kisiasa.
Lakini wanaoenda kwa mikutano ya kidini huenda kutoa pesa badala ya kutegemea kupata pesa. Kutoa sadaka au fungu maalumu ni wajibu wa kila anayeshiriki mikutano ya kidini. Ndiyo kwa maana, viongozi wa maelefu ya makanisa tilatila yaliyoko nchini ni matajiri kwelikweli waliyochuma pesa kochokocho kutoka kwa michango ya wafuasi, wengi wao wakiwa makabwela. Aidha, siku hizi kila anayehitaji utajiri wa harakaharaka hujitahidi kuwa mwanasiasa au kusajili na kufungua kanisa lake. Kisha anatajirishwa na wafuasi wa kanisa lake.
Ndiyo kwa sababu kinyang’anyiro cha wafuasi na waumini ni sehemu ya utamadini wa injili ya siku hizi. Ukweli na usemwe, kanisa limegeuzwa chombo cha matapeli cha kuchuma na kulangua wafuasi na waumini.
Lakini bado ninarudi kwa swali, kwa nini watu wengi hupendelea kushiriki katika mambo ya kidini kuliko mambo ya kisiasa? Mbona watu wengi zaidi huhudhuria mikutano ya kidini kuliko ile ya kisiasa? Nimetafakari kuhusu swali hili kwa muda mrefu na hata sasa naendelea kutafakari. Labda ni kwa vile mikutano ya kidini huwapa washiriki wao matumaini ya maisha bora na ya furaha baada ya kufa. Maisha ya ulimwenguni, hasa nchini Kenya, ni magumu na machungu mno kwa watu wengi. Watu wengi wameishi maisha haya ya shida na kusaga meno maisha yao yote. Hawajui maisha mengine ila ya dhiki na kusaga meno. Wala hawana matumaini ya kuishi maisha yoyote mengine huku ulimwenguni.
Tena wanafundishwa kuwa hapawezi kuwa na maisha yoyote bora kuliko haya ya ubepari tuliyo nayo nchini. Basi watu wanaoishi maisha bila matumaini wakihubiriwa kuhusu matumaini ya maisha ya amani na furaha baada ya kifo si wataona matumaini katika dini? Isitoshe, viongozi wa kidini hutoa suluhu za mkato: bora tu uamini na kuomba, shida zote ulizo nazo zitamalizika na unachokitaka utakipata. Na unahubiriwa vilevile kuwa ukitoa sadaka kupitia kwa kiongozi wako wa kidini basi maombi yako yatasikilizwa kwa haraka zaidi.
Kwa upande wake siasa za nchi yetu zinawakumbusha wengi kuhusu ufisadi, uongo, udhalimu, unyonyaji, wizi, utapeli, ulafi, usaliti, ujinga, uporaji wa mali ya umma na maovu tilatila yanayofanywa na uongozi. Watu wengi hupendelea mambo mepesi na ya haraka na ambayo hayahitaji kazi ngumu ya muda mrefu na ya kujitolea. Nazo siasa ya kimaendeleo ya ukombozi hufundisha kuwa ukombozi wa kuondoa maovu na kuboresha maisha ya wengi katika jamii hauwezi kupatikana bila kazi kubwa ya mapambano. Na mapambano si rahisi kwani yanahitaji watu wanaotambua utu wao ambao daima wako tayari kujitolea mhanga kwa ajili ukombozi wa nchi na wengi.
Maana hata kuwe na katiba mpya ya kitaifa – ambayo lazima ipatikane mwaka huu – hatuwezi kuona maisha bora mapya nchini bila uongozi mpya wa kimaendeleo wa kuzingatia masilahi ya kila mwananchi. Hakuna njia ya mkato. Tukiendelea kuchagua viongozi kwa misingi ya kikabila, kushawishiwa kwa pesa, kutojali na ujinga, tutasubiri hadi Yesu arudi kabla ya kuona maisha bora kwa wengi nchini.
Ndiyo kwa maana nasisitiza: ingawa katiba mpya ni muhimu sana na lazima tuipitishe kisha ikibidi tuirekebishe ama tuitupilie mbali kabisa kesho, la muhimu zaidi na la msingi ni swala la uongozi na mfumo wa kijamii – kiuchumi. Uongozi tuliyo nao leo haufai thumni nao mfumo wa kijamii – kiuchumi ni wa kupinga ukombozi madhali ni wa kufaidi wachache na kuwacha wengi pembeni katika kukwama kwa hali ya ufukara. Hivyo basi, kila anayelilia ukombozi hana budi ila kujiandikishe kuwa mpigaji kura. Tena awe tayari kupiga kura yake kwa busara mnamo mwaka wa 2012. Maana kwa wale wanaotarajia maisha bora duniani itawabidi washiriki katika harakati za ukombozi. Hakuna njia rahisi wala ya mkato. Ukombozi unadai kazi ngumu ya mapambano.
Mwandawiro Mghanga, Barua pepe: mwandawiro2002(at)yahoo.com