Makala ya Nguvu ya Hoja kwa KSB Jumapili Aprili 18, 2010
na Ndugu Mwandawiro Mghanga

Jambo muhimu sana ambalo linastahili kutajwa na makala haya limetendeka Afrika Mashariki juma hili: serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete imewapatia karibu wakimbizi mia moja wa Burundi uraia wa Tanzania. Wakimbizi hao wamekuwa wakiishi nchini Tanzania tangu makumi ya mwaka wa 1950. Kwa kuwapa haki ya kuwa wananchi wa Tanzania, serikali ya Tanzania imefanya kitendo cha kiutu cha kutekeleza haki za wakimbizi na za binadamu. Kitendo hiki kinastahili kuigwa na Kenya na nchi nyingine za Afrika na ulimwengu.
Sioni kwa nini mkimbizi halali aishi nchini kwa zaidi ya miaka mitano akitii sheria za nchi kisha anyimwe haki ya kuwa raia. Tena Mara nyingi nimekuwa nikijiuliza, Mwafrika anawezaje kuwa mkimbizi akiwa Afrika? Maana mipaka ya kitaifa iliyoko Afrika imefanywa na wakoloni. Kabla ya wakoloni wa Ulaya kuigawanya Afrika kati yao, hapakuwa na mipaka ya kitaifa. Ingawa mataifa mbalimbali ya Wafrika yaliishi na kutawala sehemu zao, hapakuwa na mipaka ya kuwazuia Wafrika kusafiri na kufanya makao pahali walipochagua.
Aliejihisi hakuwa na usalama au na maisha bora pahali alipozaliwa alikuwa huru kuhamia pahali pengine katika bara letu. Basi mbona leo nchi zetu zinazingatia mipaka tuliyoiirithi kutoka kwa mabeberu huku tukiifanya kubaguana na kunyanyasana kwa misingi ya kitaifa ndani ya Afrika na wakati huohuo tunajidai tunapigania shirikisho la Afrika Mashariki na muungano wa Afrika?
Inasikitisha kuona Mwafrika akibaguliwa ndani ya Afrika jinsi anavyobaguliwa Ulaya, Marekani na nje ya Afrika. Mimi naamini kuwa kuna haja ya kutekeleza haki za wakimbizi maana haki za wakimbizi ni haki za binadamu pia. Isitoshe, hakuna cha kupoteza kwa kuwakaribisha wageni halali nchini na hata kuwapa haki za uraia kulingana na sheria za nchi. Mara nyingi wale wageni ambao wamekuwa wakipata urai Afrika Mashariki ni matajiri wenye uwezo wa kutoa milungula kwa wakuu wa uhamiaji. Kwa sababu hii napongeza serikali ya Tanzania kwa kuwapa uraia makabwela wenye asili ya Burundi. Huu ni mwanzo mwema na mpya.
Kuhusu swala la kuwania katiba mpya: nawapongeza Rais Mwai Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga kwa kushikilia msimamo wa kuunga mkono rasimu ya katiba maana kwa kweli tunastahili kuwa na katiba mpya mwaka huu. Na madhali hatuwezi kuwa na katiba ya umalaika ambayo itatosheleza maoni na masilahi ya kila mtu binafsi nchini, tuipitishe halafu tutarekebisha mabaya yaliyoko ndani yake hatimaye. Tunaweza hata kuibadilisha katiba mpya yote siku za usoni ikiwa tutagundua haitufai kama taifa.
Ni nini kitatuzuia kufanya hivyo? Pia ni vizuri kutilia manani kampeni ya kuwasajili wapigaji kura wengi iwezekanavyo kabla ya kupigwa kwa kura za maamuzi kuhusu katiba mpya mwaka huu. Aidha, kujiandikisha kuwa mpigaji kura ni kujitayarisha kushiriki katika kuleta uongozi ambao utatafsiri na kutekeleza katiba mpya kutosheleza mambo unayoyazingatia. Usipopiga kura siyo tu utajinyima usemi wa kisiasa bali vilevile utakuwa raia mbaya.
Tukitoka hapo, Waziri Mkuu amekuwa katika ziara ya Mkoa wa Pwani na wakati ninapooandika ametembelea wilaya za Taveta na Taita. Hivyo ndivyo inapasa kufanyika maana viongozi wakitembelea watu mashinani ndipo watakapopata fursa nzuri ya kuona hali halisi na kusikiliza maoni ya wananchi moja kwa moja. Lakini ni makosa kwa viongozi waliyochaguliwa na watu kuwaficha ukweli kuhusu matatizo ya sehemu zao maana kwa kufanya hivyo hawawatendei waliyowachagua haki. Isitoshe, kuwaahidi wananchi mambo ya uongo ni dhambi.
Kwa mfano licha ya ahadi za miaka nenda miaka rudi, barabara za wilaya za Taita na Taveta ni mbaya mno na zinatatiza ajabu usafiri, biashara na uchumi. Barabara ya kutoka Voi hadi Taveta, kwa mfano, ambayo inaunganisha nchi yetu na Tanzania na Kususini mwa Afrika imeharibika kabisa na inaabisha nchi yetu kadamnasi ya majirani zetu. Miaka nenda miaka rudi kila viongozi wanapozuru sehemu hiyo huahidi kuwa itatengenezwa. Je, sasa ahadi ya Waziri Mkuu ya kutengenezwa barabara hizo itatekelezwa ama ni kilemba cha ukoka?
Tatizo kubwa katika wilaya ya Taita ni la ardhi na rasilimali zake. Wabunge wa Taita wangelimweleza Waziri Mkuu kuhusu kilio cha wananchi wa sehemu hiyo wanaodai haki za ardhi na rasilimali zinazovamiwa na kuporwa kiholela na wawekaji bandia. Ardhi za jamii zenye utajiri wa madini huingiliwa kiholela na kubinafsishwa huku wenyeji wakibaki wakichungulia mali ya ardhi yao ikisombwa na watu binafsi bila wao kushirikishwa na kufaidi chochote. Na huu ndiyo msingi wa migogoro inayoendelea Pwani. Waziri Mkuu anapaswa kufahamu ama kufahamishwa haya ili alete ufumbuzi wa mapema maana pia haya yamegusiwa na rasimu ya katiba.
Nchi yetu inaweza kuendelea kwa kasi viongozi wakiwajibika. Na kuwajibika kwa viongozi ni kufanya kazi kwa dhati kutokana na ukweli halisi. Waahidi kile wanachojua kitatendeka kulingana na hali halisi ya sasa ya kiuchumi nchini. Wafanye ziara nchini zenye lengo la kuchochea maendeleo, amani, kuwasikiliza wananchi na kushirikiana nao kutatua matatizo yanayowakumba. Ziara za viongozi wa kiserikali vilevile zisiwe ni za kujipigia debe maana kufanya hivyo ni ubadhirifu wa mali ya umma.
Mwandawiro Mghanga, Barua pepe: mwandawiro2002(at)yahoo.com
Ndugu mwandawiro mhanga jee sijui kama uko na taarifa kuhusu UAE’s new regulations require visiting Kenyans to have a degree certificate to get a visa into the Arab country. sasa kwa taswira yako unasemaje kuhusu hii issue