Makala ya Nguvu ya Hoja KSB Jumapili Aprili 4 2010
na Ndugu Mwandawiro Mghanga

Kiongozi wa Mashtaka ya Kimataifa (ICC) Luis Moreno-Ocampo juzi alipewa kibali cha kuanza kuchunguza washukiwa wa ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2007. Ghasia hizi zilisababisha vifo vya watu takribani 1300 huku zikiwafanya mamia ya maelfu ya watu kukosa makao na kuwa wakimbizi ndani ya nchi yao. Vilevile vilisababisha hasara ya mabilioni na kuyumbisha uchumi, amani na utulivu nchini pamoja na hofu na mashaka. Athari zake bado zinaendelea nchini huku wengi wakiendelea kuteseka katika kambi za wakimbizi wakikabiliwa na maisha magumu na machungu ya ufukara.
Kulingana na mashirika yasiyo ya kiserikali na hata serikali yenyewe, sehemu kubwa ya ghasia hizo zilichochewa, kupangwa na kudhaminiwa na viongozi wenye ushawishi mkubwa wa kisiasa na kiuchumi nchini na hasa katika kabila zao. Inatuhumiwa kwamba baadhi ya viongozi hao baado wangaliko serikalini wakishikilia nyadhifa kuu. Kilio cha wahanga wa ghasia za baada ya uchaguzi na kile cha wakereketwa wa haki za binadamu kinachoungwa mkono na idadi kubwa ya Wakenya kinadai haki itendeke na wahalifu wachukuliwe hatua za kisheria bila kujali kiasi cha mali ama madaraka waliyo nayo.
Utafiti umeonyesha kwamba ghasia na vita vya kikabila nchini vimekuwa vikijirudia tangu mwaka wa 1992 maana wanavyovichochea, kuvipanga na kuvidhamini hawachukuliwi hatua zozote za kisheria. Wanafanya jinsi wanavyotaka, wanaua na kuharibu mali ya wengine lakini bado wanaendelea kuwa huru huku wahanga wakilia na kusaga meno. Haya lazima yafike kikomo. Na madhali serikali imeshindwa kufanya mahakama ya kuwashtaki wahalifu wa ghasia na vita, basi wacha jumuia ya kimataifa ifanye kazi yake. Karibu Moreno-Ocampo uwasombe na kuwafungwa wahalifu hawa wanaodhani mali za wizi na ufisadi walizorithi kutoka kwa baba zao na walizopora zinawaruhusu kukanyaga na kuvunja haki za binadamu kiholela.
Maisha ni haki ya kimsingi ya kila binadamu. Kwa hivyo, tusiwe wepesi wa kuyaangamiza bali tuyaheshimu na kuyalinda kwa vyovyote vile. Maana mtu akifa ni basi! Ni muhimu kukumbuka kuwa hata hatima ya lengo la maendeleo na shughuli zote za binadamu ni kuhakikisha haki hii ya kimsingi, maisha. Chini ya mfumo wa haki na kimaendeleo wa kisiasa-kijamii-kiuchumi, shabaha ya elimu, sayansi na tekinolojia ni kumwezesha binadamu atambue utu wake na aishi muda mrefu iwezekanavyo huku akiwa na afya, amani na furaha. Vita ni vibaya kwa sababu huangamiza maisha.
Tukumbuke kuwa hata wanyama wa jamii moja hawauani, na wale wa jamii nyingine huua wa jamii isiyo yao kwa madhumuni mahususi ya kujihami au kujikimu wala siyo kiholela. Ninasikitika kusikia, kuona na kusoma kila siku kuhusu watu wanaouawa kwa kutuhumiwa kuwa wachawi, wezi, wanya’ng’anyi na kwa sababu za kila aina. Tunalaani mauaji yanaoyohusu kunyang’anyana mifugo na kushindania maliasili kama maji na machingaji hasa katika jamii za wachungaji. Basi iweje tuvumilie na kukubali watu wanaohesabiwa kuwa viongozi washiriki katika kufanya vita na kusababisha maafa na uvunjaji wa haki za binadamu waendelee kuwa huru na hata kuwa viongozi? Moreno-Ocampo fanya kazi yako tena kwa haraka kwani inaungwa mkono na katiba ya sasa na hata ile mpya itakayokuja mwaka huu.
Wala kusiwe na huruma kwa viongozi wa ghasia maana wao hawana huruma. Ikiwa watahurumiwa basi tuwahurumie wahalifu wote, tufungue milango yote ya magereza kuwafungulia wahalifu halafu tuanze upya. Utamaduni wa kinyama wa kuua watu wengine ati kwa sababu si wa kabila lako au hawapigi kura jinsi unavyotaka lazima ukomeshwe milele. Ndiyo, ni kweli kwamba kuibwa kwa kura kulizua ghadhabu na ghamu nyingi mno nchini miongoni mwa watu ambao walitarajia kuwa uchaguzi huo ungelisaidia kuimarisha demokrasi na haki za binadamu na kuweka msingi wa kusuluhisha matatizo tilatila yanayolikumba taifa letu. Pamoja na hayo yote, hatuwezi kuhalalisha kuangamizwa kwa maisha ya watu kulikotokea wakati huo, iwe ni kutokana na polisi au kutokana na raia wenyewe.
Ni kweli kuwa kuna dhuluma za kihistoria zilizoimarishwa na mfumo wa utawala ambao umekuwako tangu tupate uhuru. Dhuluma hizi zimefanya jamii nchini kuporwa haki zao juu ya ardhi na rasilimali zao na ndizo kiini cha uhasama wa kikabila na mizozo ya kila aina. Bali pamoja na hayo, hii si sababu ya kutoa haki ya maisha ya mtu mwingine ati kwa kuwa tu si wa kabila lako au unadhani amevamia ardhi ya jamii yako. Isitoshe, ukweli halisi ni kuwa makabila yote tu Wakenya.
Na tukiwa Wakenya ni lazima tulinde haki ya kila mtu ya kuishi na kuwa na mali halali pahali popote anapoamua nchini. Na ili tuishi kwa amani ni lazima tuheshimu haki na tamaduni za kila jamii. Hii ni pamoja na kutambua haki za ardhi na rasilimali za kila jamii nchini. Tukubali kwamba si sahihi ardhi na rasilimali za ardhi za jamii fulani zigawanywe bila wao kushirikishwa. Katiba mpya itumike kusuluhisha tatizo nyeti la ardhi na rasilimila zake na mahusiano yake na jamii na taifa.
Pamoja na haya yote kuua watu wengine ati kwa kuwa tu wametoka kabila tofauti na lako tena ili unyakue na kubinafsisha ardhi na mali yao kiholela au ili uhifadhi au ushinde kiti cha kisiasa si haki wala utu hata kidogo wala hakutaleta suluhisho bora na endelezi la ardhi kwa masilahi ya wengi. Ndiyo kwa maana namkaribisha Moreno-Ocampo kwa mikono miwili.
Mwandawiro Mghanga, mwandawiro2002@yahoo.com