
Kuhusu kupambana dhidi ya ufisadi hatujasonga, tungali palepale, kujiuzulu kwa makatibu wa kudumu na maafisa wengine katika wizara zinazokabiliwa na kashfa za sakata za mahindi na wizi wa pesa za elimu bila malipo, ni mawingu tu mvua bado haijanyesha. Kiangazi cha ufisadi kinaendelea kuunguza na kuharibu tu. Maana samaki akioza huanzia kichwani.
Mwenda tezi na omo marajeo ni ngamani. Sakata ya mahindi ililipuka, ikawaka na kutisha kuunguza serikali lakini kama kashfa zinginezo za ufisadi kama Anglo Leasen, Golden Bag na kadhalika siasa za ufisadi zilifaulu kuuzima moto, japo kwa muda tu. Kumbe moto wa kashfa hii haukuzimika kabisa ulibaki ukififia. Na sasa umechochewa na wanasiasa wa PNU hadi umwemuweka Waziri Mkuu katika mizani ya haki na ukweli mbele ya ufisadi. Na haya yote yamechangiwa na Raila mwenyewe ambaye alisimama kidete kadamnasi ya umma na waandishi wa habari akadai wazi na bayana wakuu wa wizara ya elimu, maprofesa Ongeri na Karega Mutahi wajiuzulu ili wawajibiki kwa niaba yao binafsi na wizara yao iliyopoteza mamia ya mamilioni ya pesa za umma kupitia kwa wizi na ufisidi uliyobobea katika wizara ya elimu.
Kumbe Raila alifungua mzinga wa nyuki. Sasa anaambiwa ajiuzulu kwani ati amekuwa kama nyani ambaye haoni kundule. Ikiwa anawataka Ongeri na Mutahi wajiuzulu mbona hajawataka Waziri wa Ardhi William Ruto na maafisa wengine wakuu wa serikali, wengine wakiwa wa afisi yake, wajiuzulu kutokana na ufisadi mkubwa wa mahindi unaohusu mabilioni ya pesa za umma? Na chambilecho Waziri wa Haki na Maswala ya Kikatiba Mutula Kilinzo, ikiwa Raila ni Waziri Mkuu kweli anaesimamia mawaziri wote wakishirikiana na Rais Kibaki, basi mbona asijiuzulu kwa kukosa au kushindwa kuchukua hatua madhubuti dhidi ya mawaziri wake wahalifu wanaoghubikwa na kashfa juu ya kashfa? Au ni siasa za kulindana za mkuki kwa kunguruwe mtamu kwa binadamu mchungu? La kukasirisha zaidi ni serikali kutoa zaidi ya milioni ishirini na kuzipatia kampuni ya kibinafsi ya Price Water House ati kufanya uchunguzi kuhusu ukweli wa sakata ya mahindini. Na taarifa ya kampuni hii imetolewa na ina sema afisi ya waziri mkuu pia inahusika na sakata ya mahindi. Kumbe mchimba kisima huingia mwenyewe!
Ninachokisema hapa ni kuwa mapambano dhidi ya ufisadi nchini zimekuwa mbio za sakafuni ambazo hazifiki kokote ila kuishia ukingoni. Maana uongo na unafiki wa viongozi unajenga ufisadi ambao siyo tu umekuwa donda ndugu lakini sehemu ya utamaduni wa Kenya. Na chimbuko chake ni tamaa ya kujilimbikizia mabilioni ya pesa na mali kana kwamba ukiwa utajiri kiasi hicho utaishi milele. Wanasahau kuwa mauko ni kwa kila kiumbe. Hata Jomo Kenyatta alikufa na kuwacha maelfu ya kilometa ya ardhi na pesa chekwachekwa.
Aidha, kiongozi bora na shujaa hakumbukwi kwa kiasi cha mali alichonyakua na kujilimbikizia bali kwa hoja na maono ya kimaendeleo na mchango wake wa kuboresha maisha katika nchi na jamii na wa kuwacha hali ya wengi na taifa ikiwa bora kuliko alivyoikuta. Ulafi umewapoteza viongozi wetu ambao wanaendelea kuaibisha na kuangamiza taifa letu kwa utovu wao wa nidhamu na adili ambao unawafanya wawe kama wanyama ambao hawana haya wala aibu. Nani atawaamini viongozi wa ndumulakuwili ambao wanasema hili leo na lingine kesho huku wakibadilisha rangi mfano vinyonga? Tumechoka na siasa potovu za ODM na PNU za kutupuuza na kutuchukulia kuwa wajinga!
Vita dhidi ya ufisadi lazima viendelee kwa vyovyote vile. Ndipo sasa tunadai serikali ya muungano iwache kabisa na mara moja kutuundia zao za kutudanganya na kuendeleza ufisadi. Kwani nchi hii in tume tilatila zilizoundwa na serikali kuchunguza mambo na kashfa zilizojaa Kenya hadi pomoni. Mabilioni ya pesa za umma zimefujwa kupitia kwa tume hizi za utapeli. Tena taarifa zinazotolewa na tume hizi ghali, nyingi zao hazitekelezwi wala hazikusudiwi kutekelezwa. Badala yake zinatumiwa kuwadanganya wananchi kuwa serikali inachukua hatua madhubuti kushughulikia jambo nyeti linalohusika. Kati yao viongozi wetu hujigamba ati taarifa za tume za uchunguzi ni kelele tu za chura ambazo kamwe haziwezi kumzuia ng’ombe kunywa maji. Ndiyo kwa maana taarifa ya Price Water House kuhusu sakata ya mahindi itakuwa kama taarifa za tume zingine za hapo awali, haina kazi wala bazi. Ni hasara tupu.
Mwandawiro Mghanga, Barua pepe: mwandawiro2002(a)yahoo.com
Lakini wewe mwandawiro utakua unatoka Tanzania !
Hicho kiswahili nadhifu na fasaha hakuna Mkenya anaweza kuongea au kuandika !
Hongera ! wafundishe kiswahili !! kitawaunganisha kama kilivyofanya Tanzania !!