From 1st January 2009, “Ukweli wa Mambo” Editions written in Kenya’s national language, Kiswahili by Comrade Mwandawiro Mghanga, at KSB will be published on Sundays. We have been carrying the Editions on Saturdays and we thank Ndugu Mwandawiro for keeping the “Ukweli wa Mambo” Edition running since it was introduced at KSB. We hope for further cooperation with Mwandawiro in the coming year and also hope that our Kiswahili readers will continue to enjoy the Edition which has been very informative and inspiring.
Makala ya Nguvu ya Hoja kwa KSB Jumapili Disemba 27, 2009
na Ndugu Mwandawiro Mghanga

Krismasi imefika. Makala haya yawatakia wasomaji popote pale walipo furaha, amani, salama na kila la heri za Krismasi. Lakini pia naomba tifikirie ukweli halisi wa maisha katika nchi yetu na kuazimia kupambana kukukuta na kuondoa unafiki na uongo ambao umekuwa sehemu ya utamaduni nchini na ambao unakuzwa, kupaliliwa na kutiliwa maji na mbolea na viongozi, wawe wa kiserikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na wa kidini.
Siku Kuu ya Krismasi, ambayo ni kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo, miaka 2009 iliyopita, hivi leo ni sehemu ya utamaduni kote ulimwenguni. Ni siku inayosherehekewa na Wakiristo, watu wa dini mbalimbali na hata makafiri. Ni wakati wa kukumbuka Yesu kwa vifijo na nderemo. Ni wakati wa ndugu, jamaa na marafiki kujumuika pamoja vijijini, nyumbani mwao, na katika sehemu na hali mbalimbali kula, kunywa na kukaa kwa furaha na bashasha.
Ni katika hali hii ambapo tunaomba usalama uwe kwa kila mtu maana kwa bahati mbaya wakati wa Krismasi pia ajali za barabara na za kila aina huongezeka na kusababisha huzuni badala ya furaha. Kwa sababu hii tunaomba kila dereva, hasa wa magari ya abiria waendeshe kwa makini na kwa kujali ili kuhifadhi usalama barabarani. Aidha, katika msimu wa Krisimasi, uhalifu na vituko vya kila aina huongezeka. Hivyo basi lazima kila raia mwema atahadhari na polisi wafanye kazi yao ya utumishi kwa watu vizuri. Lakini uwe ni utumishi wa kweli wa kulinda usalama wa raia. Usije kuwa ni utumishi wa kuzua vitimbi na kuzidisha dukuduku kwa wananchi wanaostahili amani na furaha, hasa wakati huu wa sherehe za Krismasi.
Ndiyo, ni vizuri wakati wa Krisimasi tuandae na kufurahia karamu za nyamachoma, kuku, mapochopocho na manywaji ya kila aina. Tufurahie hata kwa ngoma, nyimbo na muziki unaopendeza nyoyo zetu. Tupige gumzo na kucheka, kwani daima kucheka ni kuzuri maana kunaongeza afya. Tusafishiane nia na roho, tusameheane makosa na kujenga urafiki badala ya chuki huku tukizingatia wema wa binadamu kuliko ubaya wao. Tuombeane heri wala siyo shari, baraka wala siyo bahati mbaya. Wenye kwenda kanisani waende huku tukimkumbuka na kumuenzi Yesu Kristo kwa dhati siyo kwa chati.
Aidha, wakati tunaposherehekea tusisahau Wakenya wenzetu ambao wako katika hali ya dhiki za kila aina. Kuna wengi ambao ni mafukara ambao wanashindwa kula mlo mzuri na wa kutosha kila siku. Kuna maskwata na wale waliyotimuliwa kutoka misituni, ardhini walikokuwa wakipata ridhiki yao na sehemu mbalimabali huku wakiwachwa katika mateso bila makao. Kuna wahanga wa ghasia za baada ya uchaguzi ambao wanadidimia katika shida na mateso ya kila aina bila kujua mbele wala nyuma. Kuna ambao wameshindwa kwenda vijijini mwao kujumika na wake na watoto wao kwa kukosa nauli ama chochote cha kuwachukulia kutokana na ukosefu wa ajira ama mishahara duni.
Kuna wagonjwa mahospitalini na wafungwa magerezani ambao wanahitaji kufikiriwa kwa kila hali. Kuna wanaoishi kwa mitaa ya mabanda pamoja na magumu tilatila yaliyomo humo. Kuna walofa na mafukara wengi mijini wanaolala nje na kuishi maisha ya ombaomba. Tuwakumbuke huku tukitia manani ukweli kwamba kila mtu anastahili maisha ya kiutu, amani na furaha.
Bali tukiwawakumbuka watu waliyoko katika hali mbaya za kila aina, tusijidanganye kuwa hali zao zitabadilishwa kwa fadhila za siku moja au maombi tu. Katika historia maisha ya ufukara hayajawahi kubadilishwa na maombi matupu au sadaka za wanyonyaji. Mfumo wa kijamii – kiuchumi unaowafanya watu wengine katika jamii kuishi kwa kutegemea sadaka haufai thumni wala si wa haki au ukweli. Ndiyo kwa sababu ubepari ni unafiki. Na si vyema Wakenya tuendelee kuishi maisha yaliyoja unafiki, uongo, nyanyaso na maovu ya kila aina. Yesu Kristo daima alikuwa shujaa wa kupinga dhuluma, unafiki, uongo na kila aina ya uovu tena kwa maneno na matendo. Ndiyo kwa maana alitufundisha tuwapende jirani zetu kama tunavyojipenda sisi wenyewe. Alisisitiza kuwa ikiwa huwezi kupenda mwezako unayemuona unawezaje kumpenda Mungu ambaye hujawahi kumuona?
Kila mtu nchini anajidai kuwa Mkiristo au mwenye imani ya kidini. Bali viongozi ambao wanasema ni Wakiristo au washiriki wa dini wanafanya kazi ya kuudumisha na kuuhalalisha mfumo wa unyonyaji wa mtu kwa mtu. Tamaa ya pesa, utajiri na maisha ya kibwanyenye zimewageuza kuwa wezi, wafisadi, matapeli, waporaji wa mali ya umma, wanyakuzi wa ardhi, wapinga maendeleo na vibaraka wa wakolonimamboleo. Tamaa ya pesa pia imechafua na kunajisi kanisa la Mungu, hata Yesu Kristo akirudi leo sijui ni kanisa gani halitavunjwa na kuchomwa! Kwani wakora na matapeli wa kila aina sasa wanachumia makanisani huku wakiwafanya Wakiristo wa kweli kuwa wajinga wa kutapeliwa na kuporwa Jumapili na hata kila siku mitaani.
Hatuwezi kumkumbuka Yesu Kristo huku tukikumbatia ubepari na maadili ya kibepari. Tutamkumbuka ipasavyo kwa kutambua na kutekeleza ukweli kwamba Kenya imebarikiwa na rasilimali za kutosha kufanya kila mtu nchini aishi maisha bora ya kiutu yasiyo na dhiki na ukosefu. Bora tujipange na kuondoa mfumo wa ubepari. Mungu aliumba binadamu kwa sura yake. Na sura ya Mungu si ya ufukara wala ya ndumulakuwili – maskini na matajiri sawia. Nawatakia Krismasi njema ya mabadiliko!
Mwandawiro Mghanga, Barua pepe: mwandawiro2002(at)yahoo.com