Ukweli wa Mambo: Kura Za Maoni za Synovate Zahatarisha Demokrasi Nchini

Makala ya Nguvu ya Hoja kwa KSB Jumamosi, 14.11.2009
na Ndugu Mwandawiro Mghanga

mwandawiro

Mwandawiro Mghanga

Mfumo wa vyama vingi Kenya ulipatikana Kenya kutokana na mapambano makali na ya muda mrefu. Katika mapambano hayo, wazalendo, wakereketwa wa demokrasi na haki za binadamu waliwindwa, walikamatwa, waliteswa, walishtakiwa chini ya sheria za kiimla zilizotekelezwa na mahakama bandia, walifungwa, walilazimishwa kuwa wakimbizi wa ndani na nchi za nje na hata wengi waliuawa. Chini ya mfumo wa chama kimoja cha KANU, tawala za Jomo Kenyatta na Daniel Toroitich arap Moi zilitia fora katika kuvunja haki za binadamu za Wakenya kiholela.

Kenya ilitawalwa kama falme za watu binafsi, Marais, ndipo ufisadi, uporaji wa mali ya umma, kinyang’anyiro cha mashamba, ukabila na umbari – haya yote yakakua donda ndugu na sehemu ya utamaduni mwovu wa nchi yetu. Wakenya wakachukuliwa na Kenyatta na Moi kama watumwa ndani ya nchi yao wenyewe huku wakinyang’anywa uhuru wa kusema, kusoma, kukutana, kusambaza maoni yao na kuchagua viongozi wanaowataka. Hata Rais mstaafu Daniel Toroitich arap Moi, ambaye sasa anafurahia matunda ya demokrasi aliyoipiga vita siku zote za utawala wake, atakubaliana nami kuwa maisha chini ya mfumo wa imla wa chama kimoja yalikuwa mabaya na machungu mno kwa Wakenya. Heri haya ya mfumo wa vyama vingi.

Ndiyo kwa sababu lazima tuutetee mfumo wa vyama vingi kwa vyovyote vile. Mfumo wa demokrasi ya vyama vingi ni pato la mapambano ya umma wa Kenya. Lazima tutetee pato hili lilotokana na mapambano huku tukiendelea kudai mageuzi zaidi ya kuboresha maisha ya wengi nchini ambao bado wanaendelea kuishi maisha ya ufukara; njaa; ukosefu wa ardhi, makao na ajira; uzorotaji wa usalama; na kunyanyaswa na makabaila na mabwanyenye. Historia inatuonya kwamba tusipotetea mapato ya mapambano yetu yanayotuongezea demokrasi na uhuru zaidi, kuna hatari ya kunyang’anywa na wapinga maendeleo ambao daima wanaogopa na kuchukia ukombozi wa wengi ambao wananyonywa na kugandamizwa kwa kila hali.

Nasema hivi kwa sababu nina shaka na kura za maoni zinazotangazwa na Kundi la Synovate ambalo hutoa takwimu kuhusu wanasiasa wachache mashuhuri ati ambao ndiyo wanaotarajiwa kuwa Rais wa nchi yetu. Isitoshe, utafiti wao unaofikia uamuazi wa kusema nani kiongozi mashuhuri zaidi kadamnasi ya wananchi unaashiria kutokuwa na nia njema kwa demokrasi ya mfumo wa vyama vingi.

Siamini kuwa Synovate wanaweza kuwa wakifanya kazi ya kutoa takwimu hizi mara kwa mara bila kuwa na dhamira maalamu kuhusu uongozi wa Kenya. Katika nchi za kibepari, kile kinachoitwa kura za maoni ya wananchi ya mara kwa mara hutekeleza lengo maalumu la kuathiri fikra za raia kuhusu jambo fulani au uchaguzi kupendelea viongozi, vyama na sera fulani. Swali ni kwamba, wanaodhamini utafiti wa Synovate ni kina nani na wana nia gani?

Kulingana na ’utafiti’ wa Synovate watu wanaotarajiwa kuwa Rais wa nchi yetu ni Raila Odinga, Kalonzo Musyoka, Uhuru Kenyatta, Wiliam Ruto na Martha Karua. Swali ni, je, kwa nini Synovate waliuliza wananchi waliyowauliza kuhusu viongozi hawa tu wakati sasa kuna vyama arobaini na saba ambavyo vimesajiliwa kufungamana na Sheria ya Vyama vya Kisiasa ya 2007? Jibu la swali hili linatuelekeza tufikirie kwamba shabaha ya kura za maoni na utafiti wa Synovate ni kuwafanya Wakenya wafikirie hawana budi ila kuchagua Rais kutokana na wanasiasa hawa watano tu na vyama vyao.

Maana yake ni kwamba, hata ingawa kuna vyama vya kisiasa arobaini na saba vilivyosajiliwa, ati Wakenya watapaswa kuchagua Rais kutoka kwa ODM ama ODM – Kenya, KANU au NARC-Kenya. Hili linaogopesha! Maana ni kama kusema hakuna watu wengine Kenya ambao wanaweza kuwa Rais isipokuwa hawa tu wanaotafitiwa na kuzungumziwa na Synovate. Pia ni kana kwamba vyama vingine vya kisiasa ambavyo vinapuuzwa na Synovate haviwezi kuwa na mgombea wa Rais ambaye atafaulu kufanywa Rais na Wakenya.

Lakini ukweli ni kwamba viongozi hawa watano wanaopigiwa debe na Synovate ni sehemu ya serikali iliyoko na itikadi na siasa zao zinajulikana kwa kila Mkenya. Wao ni sehemu ya uongozi ambao umeshindwa kusuluhisha matatizo chungu nzima ya kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiusalama na kiutawala ambayo yanaendelea kuikumba nchi yetu? Wao ndiyo wanaotekeleza sera za ubinafsishaji wa kiholela wa mashirika ya umma na kuzidisha pengo kati ya matajri na maskini. Basi ikiwa itatubidi kuchagua Rais kutoka kati yao peke yake mnamo mwaka wa 2012 kuna maana tayari imeamuliwa hapatakuwa na mabadiliko ya uongozi na sera Kenya? Ati mambo yataendelea kuwa hivi hivi tu?

Maana hakuna mambo mapya yataletwa na kufanywa na kina Raila, Kalonzo, Ruto, Karua na Uhuru ambayo yamewashinda kufanya sasa wakiwa bungeni na serikalini. Swali ni, je, kwa nini utafiti wa Synovate unaendelea kusisitiza kuelekeza wananchi kuchagua Rais kutokana na wanasiasa hawa watano tu na vyama vyao tena wenye itikadi moja?

Utafiti wa Synovate hauwaoni wala hautaki kuwaona wala kuwauliza wananchi maswali kuhusu vyama vingine vya kisiasa na viongozi wao. Ndiyo kwa sababu nakariri, utafiti na Synovate na kura zake za maoni kuhusu viongozi unaelekea kupinga mfumo wa vyama vingi huku ukipendelea vyama vichache vyenye itikadi moja ya kibepari. Kenya tulipigania mfumo wa vyama vingi siyo vyama vichache. Isitoshe, ni kana kwamba ni mbinu za kuwachagulia Wakenya viongozi. Hatutaki kuchaguliwa viongozi tena, tulitoka huko zamani. Pia kura za maoni za upendeleo siyo tu zinapinga demokrasi bali zinaweza kuhatarisha amani na usalama wa kitaifa, hebu tukumbuke ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007. Tom Wolf na Synovate mwanisikia?

Mwandawiro Mghanga, Barua pepe: mwandawiro2002@yahoo.com

Mwandawiro Interview at KSB

2 comments

  • Kiswahili ni mzuri,lakini bona unaelezea na hii lugha na wengine wetu hawawezi kuelewa? Una mawazo mazuri,lakini una misamiati mingi.Kwa hivyo hueleweki.

  • Agatha Christie

    Hi there to every one, the contents existing at this web page are actually amazing for people
    knowledge, well, keep up the good work fellows. phentermine

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.