Makala ya Nguvu ya Hoja kwa KSB Jumapili Februari 14, 2010

Tume ya ukweli, haki na maridhiano inayoongozwa na Balozi Bethuel Kiplagat ivunjiliwe mbali mara moja maana haitaleta faida yoyote ile kwa taifa letu ila ahadi na propaganda za uongo na hasara tupu. Ni sehemu ya sera mbaya za unafiki na kutowajibika za serikali ya muungano za kulindana na kutafutiana kazi kupitia mapendeleo ya kirafiki, kikoo, kikabila, kisiasa na ya nipe nikupe.
Ni utapeli na ubadhirifu wa mali ya umma na kisha ni njama za wazi na bayana za kuwavisha vilemba vya ukoka wahanga wa dhuluma na uhalifu uliyotendwa na dola za imla tangu za Jomo Kenyatta na Daniel Arap Moi hadi za sasa za Rais Kibaki na Waziri Mkuu Raila. Aidha, tume hii inaweza kutumika kufunika na kuficha wahalifu waliyopanga na kudhamini ghasia za baada ya uchaguzi ambazo zilisababisha vifo, uharibifu wa mali na maisha ya wengi pamoja na vilevile kuongezeka kwa watu wasiyo na makao.
Ukweli hauwezi kupatikana na tume hii chini ya uwenyekiti wa Kiplagat anayetiliwa shaka na wananchi wengi kutokana na historia yake ya kuipiga pambaja na kuitumikia serikali ya Moi ambayo ilitia fora katika kuvunja haki za binadamu za Wakenya. Na ikiwa ukweli hauwezi kupatikana kwa sababu ya wananchi kutokuwa na imani na tume hii basi vilevile hapawezi kuwepo kwa haki na maridhiano. Hakika swara hawawezi kutarajia ukweli, haki na maridhiano kwa tume inayoendeshwa na kusimamiwa na simba mla swara.
Mahakama yanayoundwa na fisi kushughulikia kesi za mbuzi ni mahakama ya bandia. Ndiyo kwa maana mimi binafsi nikiwa mmoja wa wahanga wa mateso na unyama uliyofanyiwa Wakenya na serikali ya imla ya Moi nishamweleza Kiplagat kadamnasi ya umma awe na ujasiri siyo tu wa kukataa uwenyekiti wa tume hii bali aishauri serikali iivunjilie mbali kabisa kwa wakati huu. Kwani tatizo la tume hii siyo usimamizi mbaya tu bali hasa ni ikiwa tume hii inahitajika. Na ikiwa inahitajika ni wakati huu au ni baadae?
Historia ya nchi hii imejaa tume tilatila zilizoundwa na serikali kuchunguza mambo na kashfa mbali mbali kama zile za uvunjaji wa waki za binadamu, ghasia za kikabila, uporaji wa ardhi na mali ya umma, utumizi mbaya wa mamlaka, ufisadi na kadhalika. Mabilioni ya pesa za umma zimetumika katika tume hizi. Wasomi, wataalamu na watu mbalimbali ambao ni marafiki wa watu wenye ushawishi mkubwa serikalini wamechuma mamilioni ya pesa kutokana na tume hizi. Jambo la kusikitisha ni kuwa taarifa zinazotolewa na tume hizi ghali nyingi zao hazitekelezwi wala hazikusudiwi kutekelezwa.
Badala yake serikali hutumia tume hizi maksuudi kudanganya wananchi kuwa inachukua hatua madhubuti kushughulikia jambo nyeti linalohusika. Mara nyingi wakuu wa serikali wametajwa na taarifa za tume hizi kama wahalifu wanaostahili kuondolewa madarakani, kushtakiwa na kufungwa kutokana na ufisadi; uchochezi, upangaji na udhamini wa ghasia na vita; uvunjaji wa haki za binadamu; uporaji wa ardhi na mali ya umma; uharibifu wa misitu na mazingira; na kutowajibika ipasavyo.
Hata hivyo viongozi watuhumiwa wa uhalifu huendelea kubaki katika nyadhifa zao za uongozi huku wakiendelea kuwashauri wananchi kuhusu maadili mema ya uongozi! Hawajali maana wanafahamu kuwa kadiri wakiwa uongozini taarifa za tume za uchunguzi ni kelele tu za chura ambazo kamwe haziwezi kumzuia ng’ombe kunywa maji. Wanyonyaji na wadhalimu hawawezi kukubali kujichimbia kaburi! Hebu tazama jinsi sakata ya mahindi na ya uporaji wa pesa za elimu bila malipo inavyogeuzwa siasa za paka na panya na wakuu wa serikali wasiyo na haya wala aibu huku mamilioni ya pesa za umma zikiendelea kufujwa kwa kuleta taarifa ambazo hazina kazi wala bazi.
Kuwa na tume ya ukweli, haki na maridhiano hivi sasa ni kumaliza wakati na pesa bure na kuwapa wananchi matumaini ya uongo. Serikali yenyewe inafahamu ukweli huu. Lakini serikali iliyoko haidumu mamlakani kutokana na ukweli bali propaganda za uongo. Tume ya Kiplagat inatumiwa kama tume nyingine zinazoendelea sasa kuwarubuni wafadhili kuwa serikali inafanya mikakati ya kujenga taasisi za kushughulikia ajenda nne iliyopendekezwa na Kofi Annan katika suluhu za ghasia za baada ya uchaguzi. Ni tume ya serikali ya kujipendekeza kwa wafadhili, mabeberu, wala siyo kwa wananchi. Maana viongozi waliyoko madarakani hawajali hisia za wananchi wala maoni yao. Tume ya haki, ukweli na maridhiano haikuundiwa Wakenya. Iliundiwa macho na masikio ya wakolonimamboleo.
Tume za ukweli, haki na maridhiano huundwa baada ya kupatikana serikali yenye nia na uwezo wa kutekeleza mapendekezo ya tume hii ili kuweka msingi wa kujenga utamaduni mpya wa haki na maridhiano. Hivi ndivyo ilivyokuwa Afrika Kusuni, Sierra Leon, Rwanda, Liberia na kwingeneko. Bado tunaongozwa na serikali ambayo haina nia ya kuondoa ufisadi, uporaji wa mashamba na mali ya umma, ukabila na upendeleo, uharibifu wa misitu na mazingira na uvunjaji wa haki za binadamu. Ndiyo kwa sababu taarifa za tume mbalimbali zimepuziliwa mbali hadi sasa.
Hivyo basi, hata tume ya Kiplagat ikifaufu kuzunguka kote nchini na kusikiliza vilio vya wahanga wa utawala wa mfumo wa imla na ubepari, mapendekezo yake, hata yakiwa mazuri kiasi gani, hayataweza kutekelezwa wala hayakusudiwi kutekelezwa. Maana hakuna serikali na hali mpya Kenya yenye haja ya kurekebisha maovu yaliyofanyika. Serikali ni ileile tu ya Kenyatta na Moi, na sasa Kibaki na Raila. Basi ikiwa tume ya ukweli, haki na maridhiano inahitajika, basi tupambanie serikali na hali mpya kwanza nchini. Serikali na hali mpya ikipatikana, tume ya ukweli, haki na maridhiano huenda ikasaidia kuanza kujenga maadili mapya ya kitaifa.
Ukweli na usemwe, kuendelea kuwepo kwa tume ya Kiplagat, pamoja na tume zingine ati zinazoshughulikia ufisadi na kashfa mbalimbali, ni ufisadi na ufujaji wa maksuudi wa mali ya umma. Hata Kibaki na Raila wanajua ninasema ukweli.
Mwandawiro Mghanga, Barua pepe: mwandawiro2002(at)yahoo.com