Mfumo wa Utawala Uambatane na Mfumo wa Vyama Vingi
Makala ya Nguvu ya Hoja kwa KSB Jumapili Februari 7, 2010

Wakenya wengi wanataka kuhifadhiwa kwa mfumo wa vyama vingi. Kwani mfumo wa vyama vingi ulipatikana kutokana na mapambano makali na ya muda mrefu ya wazalendo, wengi wao wakilazimika kusakwa, kukamatwa, kuteswa, kufungwa, kuwekwa vizuizini pasina kupelekwa mahakamani, kusukumwa uhamishoni, kunyimwa haki ya ajira na hata kuuawa.
Mfumo wa vyama vingi ni pato la kidemokrasi la wananchi wa Kenya linalostahili kulindwa kwa kila hali. Nikitazama taarifa ya kamati ya bunge ya urekebishaji katiba ambayo ilikutana Naivasha kuhakiki taarifa ya wataalamu wa katiba inayoongzwa na Nzamba Kitonga, ninaona kuwa mfumo wa vyama vingi uko hatarini. Na endapo mfumo wa vyama vingi nchini ukapuuzwa, basi demokrasi yenyewe itakabaliwa na mashaka makubwa. Maana kutokana na historia dhidi ya ukoloni na imla, mfumo wa vyama vingi ni msingi wa kujenga utamaduni wa kidemokrasi na haki za binadamu.
Tena ni wa kuhakikisha amani endelevu maana unatoa fursa ya mageuzi ya serikali na utawala kufanyika kupitia kwa kura wala siyo bunduki. Hili linafaa kuzingatiwa na kamati ya wataalamu ambayo sasa inatayarisha rasimu ya mwisho ya katiba itakayopelekwa bungeni ili wabunge waijadili na kuiwasilisha kwa kura za maoni za wananchi. Wabunge nao wasiwe na pupa na papara ya kupitisha rasimu ya katiba ya kuturudisha tulikotoka. Ikumbukwe kuwa tunahitaji katiba itakayotuongezea demokrasi, haki, uhuru, amani, maendeleo na ambayo itaboresha maisha ya kila mtu na kabila nchini.
Ingawa pia inahitaji kupigwa msasa, rasimu ya katiba ya kamati ya watalamu si mbaya. Kwani ilimulika kwa kiasi kikubwa sana maoni ya wananchi yaliyokusanywa na Tume ya Urekebishaji Katiba ya Kenya na ambayo yalifikia kilele chake kwa kongamano za Bomas na kutoa katiba ya Bomas. Katika swala nyeti la utawala, Wakenya wengi walitaka mamlaka ya Rais yapunguzwe na kusambazwa kwa taasisi zingine, hasa bunge. Ndiyo kwa maana kamati ya wataalamu ikapendekeza mfumo wa utawala ambapo kutakuwa na Rais atakaekuwa mkuu wa dola na waziri mkuu ambaye atakuwa mkuu wa serikali. Katika kupiga msasa mapendekezo haya, tunaona ni bora rais asichaguliwe moja kwa moja na wananchi bali achaguliwe na bunge.
Awe karagosi wa kitaifa. Lakini waziri mkuu achaguliwe moja kwa moja na wananchi ili wakati wa uchaguzi tuwe tunapigia kura vyama pamoja na kiongozi wa vyama na sera zao. Nacho chama ambacho kitakuwa na wabunge wengi zaidi au ambacho kitafanya muungano wa vyama mkubwa zaidi ndicho kitakachounda serikali chini ya waziri mkuu mwenye mamlaka ya kusimamia serikali. Hili linamulika na kufungamana na mfumo wa vyama vingi maana chama kinachopigiwa kura nyingi zaidi na wananchi kinastahili kuunda serikali ili kitekeleze sera zake zilizopigiwa kura na wananchi kwa kipindi kinachowekwa na katiba, miaka mitano. Huu ndiyo mfumo wa ubunge. Mfumo wa ubunge unatoa fursa ya kujenga utamaduni wa demokrasi ya mapambano ya hoja na maono wala siyo ukabila na pesa.
Wabunge wameupuuza na kuutupilia mbali mfumo wa ubunge huko Naivasha. Aidha, wamependekeza kuwa haki za wafanyikazi, usalama wa kijamii, huduma za afya, nyumba, chakula, maji, haki katika sheria, lugha na utamaduni zisiwe haki za kikatiba. Si ajabu kwamba wengi wa wabunge hao hawajawahi kushiriki katika harakati za kidemokrasi na haki za binadamu nchini. Badala yake walikuwa wakiupigia debe udikteta huku wakipinga mfumo wa vyama vingi. Walikuwa wakichuma mali kupitia kwa mfumo wa ufisadi, uporaji, ukabila, upendeleo, unyonyaji na udhalimu. Wengine wao wako siasani kutetea mashamba na mali ya wizi waliyonyakua na kurithi kutoka kwa baba zao. Wana harakati wachache waliyokuwako Naivasha walishawishika kuunga mkono njama hizi dhidi ya demokrasi maksuudi.
Dunia ni mduara, waliyokuwa wakipinga marekebisho ya kikatiba sasa ati ndiyo wanaotuandikia katiba. Huku wakitumia propaganda kupitia kwa vyombo vya habari, wanapigia debe rais ambaye atakuwa na mamlaka kama ya mfalme. Zaidi ya mamlaka makubwa mno aliyo nayo katika katiba ya sasa, kamati ya wabunge huko Naivasha imemuongezea uwezo wa kuchagua mawaziri kutoka nje ya bunge. Yanayosemwa ati wabunge wataathiri uteuzi wa rais ni porojo tupu katika hali halisi maana mawaziri hawa ambao si lazima watokane na vyama vya kisiasa, watawajibika kwa rais tu wala siyo kwa vyama, itikadi wala sera. Rais naye hatawajibika moja kwa moja kwa bunge, chama cha kisiasa au sera za chama. Atatawala tu kama mfalme kutoka ikulu.
Je, kamati ya Nzamba Kitonga inaweza kuokoa jahazi kwa kuwa na ujasiri ya kuchuja na kuchekecha maoni ya kamati ya wabunge kama maoni ya Wakenya wowote wale katika kuandika rasimu ya mwisho itakayowasilishwa bungeni?
Mwandawiro Mghanga, Barua pepe: mwandawiro2002(at)yahoo.com