Makala ya Nguvu ya Hoja kwa KSB Jumapili Januari 31, 2009
na Ndugu Mwandawiro Mghanga

Sasa ya mno. Hatuwuwezi kuvumilia tena. Sharti serikali ya Rais Mwai Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga iwajibike. Lazima tuelezwe kinagaubaga ni nani hasa ambaye ameiba pesa za kuhakikisha kuwa idadi kubwa ya watoto nchini wanapata fursa ya kupata elimu ya msingi na hata ya upili kupitia kwa mpango wa ruzuku maalumu inayotolewa na serikali. Sasa ruzuku hiyo imeibwa na mafisaa wa serikali wenyewe na hivi sasa maelfu ya watoto kote nchini wako katika hatari ya kukosa elimu.
Na hata wakipata elimu, itakuwa ni elimu bure maana hakuna fedha za kugharamia mahitaji ya elimu bora, hasa kwa watoto wa wananchi wengi ambao ni makabwela na mafukara. Kwani serikali za Wingereza na Marekani ambazo zinatoa fedha nyingi za kugharamia ruzuku ya elimu ya kuhakikisha kuwa kila mtoto ana fursa ya angalawa kuenda darasani zimeamua kusitisha kutoa misaada yao. Nami nakubaliana nao, wanawezaje kuendelea kutoa pesa ambazo hazifikii lengo lake na badala yake zinaibwa na watu serikalini ambao wanakua mamilionea kwa uporaji na ufisadi huu.
Umma wa Kenya unastahili kukasirika zaidi kuliko wafadhili. Kwanza ni makosa kwa serikali kuendelea kufanya mipango ya elimu inayotegemea kuendeshwa na wafadhili wa kigeni. Pili ni vibaya kwamba hadi sasa hakuna hatua yoyote ile iliyochukuliwa na serikali dhidi ya wale waliyoiba pesa hizi. Na tusiambiwe kwamba wezi hawa katika idara ya elimu na kwingineko hawajulikani. Polisi wapo; kitengo cha polisi cha uchunguzi wa uhalifu (CID) kipo; taasi ya huduma za ujasusi wa kitaifa (NIS) ipo; afisi ya mkuu wa sheria ipo; macho ya wananchi yapo; na hata tume ya kupambana dhidi ufisadi ipo – taasisi zote hizi haziwezi kushindwa kujua ni nani aliyeiba pesa za serikali. Je, pamoja na ukweli huu mbona serikali ya Kibaki na Raila inakataa kuwachukulia hatua wanaohusika?
Mbona inaendelea kuwalinda wezi na matapeli wakati raia wanaumia? Au ni kwa sababu watoto na wajukuu wao ambao wanasoma shule za kibinafsi hawana shida? Ina maana gani kuendelea kuwa na serikali ambayo imejaa ufisadi na wafisadi? Lazima Kibaki na Raila wawajibike mara moja, wala hatuwezi kukubali waendelee kujitia hamnazo na kupuuza maoni yetu.
Hatua iliyochukuliwa na serikali ya kutumia shilingi milioni arobaini kumahamisha Sheilk Abdullah al Faisal kutoka Kenya hadi Jamaica ni ya ujinga, utapeli na ya ufujaji wa pesa za umma. Wala si dhani inakusudiwa kulinda usalama wa kitaifa kuliko kujipendekeza kwa mabeberu wa kimataifa na kuhatarisha usalama wa nchi yetu kwa sababu ambazo hatujui. Si wezi kumuhukumu raia huyo wa Jamaica kwa kuwa tu tumeambiwa na mabeberu kuwa yuko kwa orodha ya magaidi. Orodha yenyewe imefanywa na nani na ina ukweli gani? Hatujaelezwa Faisal amefanya nini, lini na wapi ndipo akawekwa katika orodha ya watu hatari ulimwenguni? Na ikiwa ni gaidi hatari jinsi tunavyoambiwa, mbona yuko huru nchini kwao Jamaica na aliingia nchini kwetu kihalali na akafanya mambo yake hadharani bila kuvunja sheria za nchi yetu. Mbona serikali inataka kutufanya taifa la kuvunja haki za binadamu wanaotembelea nchi yetu. Mbona serikali hii inafanya mikakati ya usalama kutokana na uvumi unaoenezwa na wakolonimamboleo? Wageni wanaostahili kuchukuliwa hatua ni wale wanaonyemelea na kuingia nchini na kuishi bila kujitambulisha kwa serikali. Aidha, hakuna serikali au mtu yoyote mwema anaependelea ugaidi na magaidi.
Lakini kumpachika mtu jina la ugaidi bila ushahidi wowote na kumdhulumu bure ni kitendo ambacho hakiwezi kuvumiliwa na wale wenye busara na ustarabu. Katika hatua za kishenzi na uhange za kukabiliana na Faisal, ambazo zilizua zogo lililosababisha maafa, majeraha, uharibifu wa mali na watu kukamatwa na kufungwa, waliyofurahia ni nani? Ni al-Shababu ambao walifaidi kipropaganda kwa kutangazwa kwamba wana wafuasi Kenya na uwezo wa kusababisha na kuathiri mambo Nairobi. Kisha biashara ya utalii Kenya ikazidi kupata madhara kutokana na sera za kiusalama za kijinga za serikali ya Kibaki na Raila.
Nayo yanayofanya na wabunge Naivasha ni wazimu mtupu. Si ajabu kuwa wengi wa wabunge wanaoshughulikia urekebishaji wa katiba huko Naivasha ni watu ambao hawajashiriki katika harakati za kidemokrasi nchini tangu uhuru. Ni watu ambao walikuwa viongozi wa serikali ya imla na walichuma mabilioni kutokana na ufisadi, ukabila na uporaji wa mali ya umma uliyokuwa ukiendelea katia serikali za KANU za Kenyatta na Moi. Wengi wa wabunge wanaojitia kutuandikia katiba ni wale waliyorithi mali na mashamba ya wizi kutoka kwa baba zao na wanaoendelea na utamaduni wa ubakuaji. Na huku wachache waliyokuwa wazalendo jana wakiangalia na kukubali, wanyonyaji na wapinga maendeleo wanafanya kazi ya kuandika katiba ya kulinda na kuendeleza utamaduni wa imla, unyonyaji, uporaji na uvunjaji wa hali za binadamu. Wako tayari kutilia manani maoni ya mabeberu kuliko yale ya wananchi wa Kenya. Ni wasaliti.
Wala hakuna aliyewatuma Naivasha kutuandikia katiba. Kazi hii ilifanywa kitambo na wananchi wenyewe kitambo hadi kufikia kilele chake kwa kongamano za Bomazi na uainishaji na Kamati ya Wataalamu. Wamefanya kazi ambayo si yao na wakavuruga na kuharibu kilelelezo cha katiba. Badala ya mfumo wa urais uliyoko sasa wamependekeza mfumo wa urais wa kifalme.
Wameondoa haki halisi za binadamu, utamaduni wa kitaifa, tume ya ardhi, haki za jamii juu ya ardhi zao na mengi ya kulinda haki za wengi ambao ni mafukara. Kwa vile ni matajiri na wana wa waporaji wanahakikisha katiba italinda mali ya binafsi na kupinga mali ya umma. Wengine hata wamethubutu kupendekeza kuwa katiba inayoandikwa Naivasha ipitishwe bungeni na iwe katiba mpya ya kitaifa pasina kura zamaoni. Tupende tusipende. Lo, kumbe harakati urekebishaji katiba hazijakaribia kuisha!
Mwandawiro Mghanga, Barua pepe: mwandawiro2002(at)yahoo.com
And if thy dont want…let them wok….