Je, Unaikubali Katiba Pendekezo ya Kenya? Jibu Langu ni Ndiyo!
Makala ya Nguvu ya Hoja kwa KSB Jumapili Mei 16, 2010
na Ndugu Mwandawiro Mghanga
Bila shaka penye wengi pana mengi. Huku tukikaribia kabisa kupata katiba mpya ya kitaifa wengine wamesuka vitimbi vya kuvuruga mambo. Je, ni nani aliyepanga njama za kuingiza maneno bandia “kwa ajili ya usalama wa nchi” kwenye kifungu 24 (1.d) katika katiba mpya ya Kenya inayopendekezwa? Alitumwa na nani? Alishirikiana na nani? Alikuwa na nia gani? Haya ndiyo maswali ambayo yanaulizwa na wananchi tangu njama hizi za kihaini zigunduliwe na kutangazwa. Tuna haki ya kupata majibu ya maswali haya kwani waliyofanya uhalifu huu ndiyo watu wa kwanza kupinga katiba mpya kinyume cha sheria. Wala si watu wenye msimamo, wangelikuwa na msimamo wangelijitokeza wazi na bayana kuipinga katiba na kifungo kinachohusika kwa kutoa hoja za haja badala ya kutujaza vioja tusivyovihitaji wakati huu.
Kuna fursa kwa kila mtu kusoma, kujadili na kufanya maamuzi ya ndiyo au la katika kura za maamuzi zitakazofanyika hivi pindi mwakani. Basi mtu ana sababu gani kutumia ulaghai ambao unasababisha hofu, mashaka na dukuduku miongoni mwa raia na hasara kubwa za fedha za umma? Je, ni nani atalipa gharama za nakala potofu za katiba bandia? Lazima waliyopanga njama hizi za uhaini wakamatwe. Naamini serikali ina taasisi za kutosha kufichua ukweli wa jambo hili ikiazimia kufanya hivyo.
Wahalifu hawa hawawezi kuwa wananchi wa kawaida. Ni watu ambao wanapinga demokrasi na haki za binadamu kama zilivyo katika katiba pendekezo. Maana kuingiza maneno ”kwa ajili ya usalama” katika kifungo 24 (1.d) ni kupinga haki za binadamu zilizoodhoreshwa katika katiba pendekezo. Ni kupanda mbegu za imla. Ni kuturudisha nyuma katika hali ambapo tumekuwa tukinyanyaswa ”kwa ajili ya usalama wa kitaifa”. Kwa ”ajili ya usalama wa kitaifa” maandamano halali na ya amani ya wananchi yamekuwa yakivurugwa na polisi na haki za binadamu kuvunjwa kiholela”.
Wengi, nikiwemo, wamesakwa, wamekamatwa, wameteswa, wamefungwa, wamewekwa vizuizini, wamefukuzwa kutoka vyuo vya elimu, kufutwa kazi – yote hayo kwa ”ajili ya usalama kwa kitaifa”. Hii ilikuwa ni mbinu ya wakoloni ya kuwadhulumu Wafrika ambayo ilifanywa sehemu ya katiba na sheria, kisha ikatumiwa na viongozi waliyochukua nafasi ya wakoloni kuimarisha ukplonimamboleo na utawala wao wa kiimla wa giza, vitisho na vifo. Kwa ”ajili ya usalama wa kitaifa” imetumiwa kuchelewesha kupatikana kwa mfumo wa vyama vingi na kuupalilia ufisadi. Na sasa wenye nia ya kuturudisha kwa udikteta walisuka njama ya kuitumia kuhujumu mapato ya kidemokrasi, uhuru na haki za binadamu ambayo tumejishindia katika katiba pendekezo ya Kenya. Pongezi kwa hao waliyogundua na kufichua ufidhuli huu. Kumbe Kenya kuna wazalendo.
Pamoja na hayo, safari ya kuelekea kwa katiba mpya lazima iendelee. Isisimame hata kwa sekunde moja. Wanaopinga katiba pendekezo wasitumie uhalifu uliyotendeka kama sababu ya kupinga juhudi za kupatikana kwa katiba mwaka huu. Ingawa tunatarajia kufichuliwa kwa ukweli kuhusu uhalifu uliyofanyika, swali la msingi sasa ni ”Je, unakubaliana na katiba pendekezo ya Kenya?” Hilo ndilo swali tunalotarajiwa kujibu katika kura ya maamuzi. Mimi nitapiga kura ya kusema NDIYO. Maana nimeisubiri katiba mpya kwa muda mrefu mno; nimeshiriki katika kuipambania; nimekumbana na mengi magumu na machungu kwa ajili ya katiba mpya; nimepoteza ndugu, jamaa na marafiki kwa ajili ya demokrasi, haki za binadamu na katiba mpya; mabilioni ya kodi zetu yametumiwa kuitafuta katiba mpya mwaka nenda mwaka rudi. Na sasa siko tayari kuchangia katika kukosekana kwa katiba mpya wakati ikiwa imekaribia kabisa. Isitoshe, nimeisoma na naendelea kuisoma katiba pendekezo na naona inafaa.
Ingawa kuna mambo kadhaa ambayo sikubaliana nayo lakini mambo mengi sana na zaidi katika katiba pendekezo ni mazuri. Tena uhuru na ukombozi haupatikani wote mara moja au kwa siku moja. Ni hatua kwa hatua katika mwenendo wa mbele daima. Ninasema NDIYO kwa katiba pendekezo maana imetufikisha mbali sana kama Wakenya na binadamu katika safari ya kidemokrasi, uhuru, haki za binadamu, umoja wa kitaifa na maendeleo endelevu.
Katiba pendekezo ya Kenya imetufikisha katika swali, ”Je, ni mfumo gani wa kijamii – kiuchumi” utakaoweza kutekeleza orodha ndefu ya haki za binadamu zilizoko ndani ya katiba mpya tunayoitarajia? Ni viongozi gani ambao wataweza kuitafsiri na kuitekeleza katiba mpya kuleta mambo mapya ya kuboresha maisha ya wengi nchini. Ndiposa ninanakariri tuseme NDIYO kwa katiba pendekezo ya Kenya ili tupate katiba mpya mwaka huu kisha tuanze harakati zenyewe hasa za kuitumia katiba mpya kusawazisha mambo, harakati za kitabaka.
Ni harakati za kitabaka zilizotufikisha hapa kikatiba leo na ni harakati za kitabaka zitakazoendelea kulizungusha mbele gurudumu la maendeleo baada ya kuwasili kwa katiba mpya. Tusisahau kwamba kura za mwaka wa 2012 ndizo zitaamua ikiwa kweli katiba mpya itaanza kutumika kuanza kufanya maendeleo endelevu yanayozingatia haki za binadamu zilizoko katika katiba pendekezo. Ndiyo, sote tuseme NDIYO Kenya ipate kusonga mbele.
Mwandawiro Mghanga, Barua pepe: mwandawiro2002(at)yahoo.com




