Makala ya Nguvu ya Hoja kwa KSB Jumapili Machi 21, 2010
na Ndugu Mwandawiro Mghanga

Wabunge sasa wanajadiliana kuhusu hatima ya mwisho ya kielelezo cha katiba kitakachojadiliwa bungeni kisha kipelekwe kwa kura za maoni. Mkutano huu unafanyika katika Taasisi ya Utawala ya Kenya (KIA) huko Kabete. Kwanza nawapongeza kwa kuamua kufanya mkutano huo katika taasisi ya serikali badala ya zile za kibinafsi ambazo hutumiwa mara kwa mara. Kuna maana gani tujenge taasisi za serikali zenye uwezo wa kufanya mikutano mikubwa kama hiyo halafu tutumie pesa za serikali kwa zile za kibinafsi? Si huko ni kuhujumu juhudi za taasisi za umma?
Kwa wabungu kulitilia manani swala la katiba mpya ni jambo hili ni la kutia moyo. Matumaini yangu ni kwamba mijadala yote kuhusu katiba iwe na nia ya kuhakikisha tunapata Katiba mpya mapema mwaka huu. Maana tumeingojea Katiba mpya kwa muda mrefu mno. Wala hatutaki tuendele kuingojea zaidi.
Tunataka tumalize swala la Katiba mpya ili tuanze kuitekeleza ifanye kazi halisi ya kutuwezesha kupambania mfumo wa kijamii – kiuchumi utakaotupa uwezo wa kutumia rasilimali za watu na maliasili tulizo nazo kuhakikisha tunaendelea kiuchumi, kisiasa, kijamii na kitamaduni; tunaondoa umaskini na unyonyaji wa mtu kwa mtu; tunajenga utamaduni wa kidemokrasi na haki za binadamu; tunaimarisha usalama, amani na umoja wa kitaifa; tunajali na kuhifadhi mazingira; tunalinda uhuru wa taifa letu na wa kujiamulia sudi yetu sisi wenyewe; tunakuwa na utawala bora wa kuondoa ufisadi na kuhakikisha matumizi mazuri ya pesa na mali ya umma; tunajenga mfumo bora wa haki na sheria; na tunatambua na kutekeleza masilahi ya kila kabila, kundi na mtu katika jamii tangu watoto, vijana, wazee, walemavu, wanawake na wanaume. Nionavyo mimi Katiba Kielelezo kwa ujumla imefaulu kuweka msingi imara wa kujenga taifa mpya la Kenya na ndiyo ninapendekeza kuwa mijadala inayoendelea isilenge kuangusha Katiba Kielelezo bali iwe na shabaha ya kuipiga msasa Katiba Kielelezo ili iwe Katiba mpya ya kitaifa mwaka ujao, 2010.
Ninakariri tena: Katiba si Bibilia Takatifu au Korani Takatifu. Hivyo tusitumie uhai wetu wote kutafuta katiba ya umalaika ambayo haiwezi kupatikana. Isitoshe, tusidanganye kuwa kila mtu Kenya atashiriki katika kujadili na kupitisha Katiba Kielelezo. Hili kwa kweli haliwezikani. Kwani ni gharama kubwa mno na isiyo na mantiki kutengeneza nakala za kutosha kusomwa na takribani milioni arobaini ya Wakenya. Fauka ya haya, wengi ni watoto, watu wasiyojua kusoma na kuandika na ambao hawawezi kushiriki kikamilifu kwa mjadala kuhusu Katiba kwa sababu mbalimbali. Ndiyo kwa maana ni muhimu kwa wale wenye uwezo wa kushiriki katika mjadala wa Katiba Kielelezo na watakaopatia umma elimu kuhusu Katiba Kielelezo wafanye hivyo kwa kuzingatia ukweli, maadili ya kitaluma, uzalendo, kujenga mwafaka, haki na nia ya kufikia Katiba Mpya mapema mwaka ujao. Pia tukumbuke kila mara kuwa Katiba Mpya ambayo iko karibu kupatikana, itapatikana kutokana na kutengeneza mwafaka kabla ya kufanyika kwa kura za maoni, na hasa kushughulikia kikamilifu maswala nyeti ambayo bado yanaendelea kuzua utata.
Sioni kwa nini swala la Mahakama ya Kadhi linaendelea kuzua utata. Mahakama ya Kadhi yamekuwako nchini yakishughulikia mambo ya ndoa na miradhi ya Waislamu kwa mda mrefu. Jamii ya Waislamu wenyewe wanayapenda na kuyahitaji mahakama ya Kadhi ambayo hayaingilii haki za dini nyingine au watu wengine nchini. Wala hayako juu ya Katiba na pia hayakinzani na mfumo wa haki na sheria wa Kenya. Aidha, Katiba mpya inakusudiwa kuongeza wala siyo kupunguza haki. Kwa sababu hii kutambuliwa kwa Mahakama ya Kadhi na Katiba Kielelezo ni jambo nzuri na halifai kutumiwa kama kisingizio cha kutuzuia kupatikana kwa Katiba Mpya haraka iwezekanavyo.
Ilivyoko sasa wabunge wamependekeza mfumo wa utawala wa Urais. Kulingana na mapendekezo hayo yaliyotoka kwa kongamano la kwanza la wabunge wanaoshughulikia katiba lililofanyika huko Naivasha, Rais alipewa mamlaka makubwa mno. Kwangu mimi Rais anayependekezwa ni kama mfalme ambayo ana mamlaka makubwa kuliko aliyo nayo katika katiba ya sasa. Isitoshe, baadhi ya wabunge wanataka awe na mamlaka hata zaidi. Hili kwangu linanitia hofu na wasiwasi kwani hakuna demokrasi chini ya utawala wa kifalme. Naogopa hasa kwa sababu minapendelea mfumo wa utawala wa ubunge maana ndiyo wa kidemokrasi zaidi na ndiyo uliyopo kwa nchi nyingi zaidi zenye mfumo wa vyama vingi kama za Ulaya, Urusi, India, Indonesia, Israel na kadhalika.
Bali wahenga pia walisema wengi wape, hatuwezi kujadili kuhusu katiba milele. Basi tuipitishe katiba mpya hata ikiwa ni ya mfumo wa uraisi wa kifalme. Nayo iaandamane na ung’atuzi wa kweli wa kimajimbo na baraza la seneti lenyeuwezo mkubwa wa kuhakikisha ung’atuzi unatekelezwa. Hali halisi ya utekelezafi wa katiba yenyewe itatufunza ikiwa inafaa au haifai. Kama haifai hakuna kitakacho tuzuia kuibadilisha au kuirekebisha. Wacha ije.
Mwandawiro Mghanga, Barua pepe: mwandawiro2002(at)yahoo.com
Tena na tena untoboa ukweli kwa kiswahili fasaha
we as kenyans have struggled and prayed for a very long time for a new cnstitiution and i think and believe that this is right time for kenyans tohave it and that can only be achieved by voting YES to katiba mpya.