Makala ya Nguvu ya Hoja, KSB Jumapili Februari 28, 2010
na Ndugu Mwandawiro Mghanga

Uhalifu ni uhalifu, uwe umetendwa na tajiri au maskini; uwe unahusu viongozi au wananchi wa kawaida. Tena wenye kutilia manani haki husema sheria ni kama msumeno ambao hukata mbele na nyuma. Kwa nini nchini Kenya sheria iendelee kutekelezwa dhidi ya uhalifu unaofanywa na wananchi wengi, hasa mafukara, wakati ambapo inasitasita ikifikia uhalifu unaotendwa na viongozi au watu wenye ushawishi mkubwa wa kisiasa na kiuchumi? Mbona tuendelee kuruhusu taasisi zilizoundwa kuhakikisha utawala wa kihaki na kisheria ziendelee kutumika kwa njia za kibaguzi huku zikiwalinda na kuwahurumia wahalifu wakuu wenye mamlaka makuu na wa kutoka tabaka kuu?
Ninasema hivi maana naona ni wazi na bayana kuwa utamaduni wa uhalifu unaochukua mwelekeo wa kitbaka na mara nyingi unaofanana na ule wa kimafia umepaliliwa na kutiliwa mbolea nchini tangu kale na zamani. Wizi, hata uwe wa yai, ukiwahusu makabwela au walalahoi unaitwa wizi na watuhumiwa wanakamatwa na polisi mara moja na kupelekwa mahakamani na kisha wakipatikana na hatia wanahukumiwa na kufungwa gerezani. Ndiyo kwa maana magereza ya nchi yetu yamefurikana na maelfu ya watu kutoka tabaka la makabwela ambao wamepatikana na hatia ya kuvunja sheria.
Lakini wizi ukitendwa na vigogo, watu wenye ushawishi mkubwa wa kisiasa na kiuchumi au viongozi, hauitwi wizi tena, unaitwa ufisadi. Nalo neno la ufisadi limekuwa utamaduni wa kufunika na kuupatia hadhi uhalifu unaotendwa na viongozi na matajiri. Ufisadi umekuwa uhalifu wa wenye kutunga sheria za kupambana dhidi ya uhalifu ambao unachukuliwa na kushughuliwa tofauti na ule wa makabwela. Wakati ambapo uhalifu wa makabwela unashughulikwa na polisi mara moja, ule wa viongozi na wenye ushawishi unashughulikiwa na tume ya kupambana dhidi ya ufisadi. Isitoshe, uhalifu wa viongozi na wenye ushawishi haushughulikiwi mara moja, huchukua miaka na mikaka na mara nyingi waliyohusika huepuka mkono wa sheria baada ya mamilioni ya pesa za umma kutumiwa kwa uchunguzi wa ’ufisadi’ waliyoutenda.
Katika kupambana dhidi ya uhalifu lazima tuwe tayari kuita uhalifu kwa jina lake. Wizi uwe wizi, unyang’anyi uwe unyang’anyi, uporaji wa mali ya umma uwe uporaji wa mali ya umma. Wala sioni haja ya tume ya kupambana dhidi ya ufisadi katika nchi yenye sheria na taasisi maalumu za kupambana dhidi ya uhalifu wowote ule. Tume hii inatumia mabilioni ya pesa za umma bure bulashi. Polisi, wakishirikiana na afisi ya mkuu wa sheria, mahakama na wizara ya haki, wanasatahili kuwa na uwezo ama kupewa uwezo wa kupambana kikamilifu dhidi ya uhalifu popote pale unapopatikana na pasina ubaguzi. Mbinu za kubatiza wizi na uhalifu wa viongozi na wenye ushawishi ufisadi ukome ili wezi na wahalifu wengine washughulikiwe ipasavyo bila kuwalinda kwa jina la ufisadi.
Makala haya yamekariri mara nyingi kuwa mawaziri wanaotuhumiwa kushiriki wizi wanga’atuke ama wang’atuliwe. Kuendelea kukubali watuhumiwa wa wizi wa mali ya umma kuendelea kushikilia nyadhifa za uongozi wa kitaifa ni kupalilia na kutilia mbolea uhalifu. Aidha, serikali ambayo inalinda wahalifu siyo tu haiwezi kuaminika bali pia inaaibisha nchi yetu na kuhujumu juhudi za wananchi za kujikomboa kutoka kwa umaskini ambao unakua siku nenda siku rudi.
Ada ya mja husema, mungwana ni vitendo. Ikiwa wewe ni waziri na umetuhumiwa kwa uhalifu, basi jambo la kingwana ni kujiuzulu kisha ungojee uchunguzi ufanyike na mahakama yaamue kama una hatia au la, jinsi maafisa wanaohudumu chini yako walivyofanya. Maana ni wazi kuwa kadiri ambapo unashikilia mamalaka ya uwaziri unazuia uchunguzi kufanyika na ukweli kujulikana. Isitoshe, utaambia wananchi kitu gani kuhusu uhalifu ikiwa wewe mwenyewe ni mtuhumiwa wa uhalifu?
Mja muue na haki umpe. Waziri Mkuu Raila amefanya jambo la ujasiri. Aliwafuta kazi mawaziri waliyotuhumiwa kwa wizi wa mali ya umma. Bali Rais Kibaki amekataa na mawaziri wake. Na kumbe mamlaka ya Raila ya uwaziri mkuu ni mamlaka ya nyuma ya chupa. Mamlaka yenyewe hasa yako na Kibaki. Ndiyo kwa maana Ongeri na Ruto bado ni mawaziri, wamemshinda Raila na wanaendelea kumcheka na kumkebehi. Lakini mimi nafikiri anaechekwa na kukebehiwa siyo Raila bali ni wananchi wa Kenya. Tunaambiwa kuwa tutasema mchana lakini usiku tutalala. Kisha kelele za chura hazimzuii ng’ombe kunywa maji. Kwani maslahi ya kisiasa, ushawishi wa kitabaka na utamaduni wa kubatiza uhalifu kuwa ufisadi utaendelea kuhakikisha watuhumiwa wa ufisadi wanaendelea kuwa viongozi – tupende tusipende. Aidha, hata wananchi wenyewe wako tayari kutetea, kulinda na kupigania wahalifu wa kutoka kabila zao. Masikitiko!
Mwandawiro Mghanga, Barua pepe: mwandawiro2002(at)yahoo.com